2016-02-24 07:56:00

Toba na wongofu wa ndani ni chachu ya mabadiliko!


Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria katika mkutano wake wa mwaka uliofanyika hivi karibuni ukiongozwa na kauli mbiu “Kanisa Katoliki: Kuendeleza huruma, haki jamii na amani”, limesema, ili kupata suluhu ya matatizo na changamoto mbali mbali zinazoendelea kuwaandama wananchi wa Nigeria, kuna haja kwa Mama Kanisa kujikita katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kuongoa roho za watu, tayari kuambata huruma, haki jamii na amani ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha mwanadamu!

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Nigeria wanapaswa kuanza kuwa na mwelekeo chanya katika maisha badala ya kujifungia katika woga na wasi wasi wa mashambulizi ya kigaidi ambayo kwa miaka ya hivi karibuni yamewatikisa na kuwadhalilisha sana wananchi wa Nigeria. Wananchi wajifunge kibwebwe ili kupambana na changamoto za kiuchumi, kijamii na kisiasa huku wakiendelea kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa na kamwe wasikubali kugawanyika kwa misingi ya umajimbo, udini na ukabila, mambo ambayo hayana tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wa Nigeria katika ujumla wao.

Ili kuweza kuwa na mweleko wa Nigeria mpya anasema Askofu mkuu Ignatius Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, wananchi wanatakiwa kujikita katika kanuni maadili, sheria na taratibu za nchi. Wawe ni watu wanaothubutu kumwilisha mambo mema katika jamii kwa kujikita katika haki, amani na utulivu. Wananchi wawe na mwamko mpya katika dhamiri zao, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini ya ujenzi wa Nigeria mpya. Wananchi wajenge mazingira bora zaidi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watoto wao kwa siku za usoni; kwa kujikita katika Injili ya uhai na kukataa kushabikia utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sheria za utoaji mimba na vitendo vya kigaidi. Taasisi mbali mbali na Serikali katika ujumla wake, wawe mstari wa mbele katika ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Nigeria.

Askofu mkuu Kaigama anasema, ili Nigeria iweze kucharuka katika misingi ya haki, amani na maridhiano, kuna haja ya kuivalia njuga saratani ya rushwa na ufisadi ambayo imepelekea Nigeria kufika mahali ilipofikia kwa kukosa amani na utulivu; kwa kuendelea kurudi nyuma katika maendeleo na wananchi wake wengi kutumbukia katika umaskini wa hali na kipato. Wafanyakazi wa umma wawe waadilifu na makini; watu wanaoongozwa na sheria, kanuni maadili na taratibu za nchi na kamwe wasitake kutumia njia za mkato ili kupata mafanikio katika maisha.

Kuna wananchi wachache sana nchini Nigeria ambao wamejikusanyia utajiri wa mkubwa kwa gharama na mateso ya wananchi wengi wa Nigeria. Uongozi ni huduma na wala si kichaka cha kujikusanyia fedha na utajiri. Kwa kumezwa na uchu wa mali na madaraka, baadhi yaviongozi wamesababisha umaskini mkubwa kwa wananchi wa Nigeria, kwani viongozi wachache wameamua kujitajirisha kwa kutumia mgongo wa wananchi wengi wa Nigeria. Umefika wakati wa kuwekeza katika maeneo ambayo yatasaidia kutoa fursa ya ajira kwa wananchi wengi wa Nigeria kwa kuhakikisha kwamba, Nigeria inakuwa na uhakika na usalama wa chakula kwa watu wake. Kilimo katika miaka ya hivi karibuni hakikupewa msukumo wa pekee. Pengine umefika wakati wa kuwekeza katika sekta ya kilimo badala ya ununuzi wa silaha zinazosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Nigeria inapaswa kutafuta vyanzo vingine vya pato la taifa badala yakutegemea kwa kiasi kikubwa biashara ya nishati ya mafuta ambalo soko lake duniani linaendelea kuyumba kana kwamba, ni “daladala” iliyokatika usukani! Rasilimali na utajiri wa nchi ni mambo yanayopaswa kutumiwa kwa busara, uaminifu na kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi na wala si kwa ajili ya kuwatajirisha watu wachache katika jamii. Wananchi wa Nigeria kamwe wasikubali kumezwa na mipasuko ya kidini, kijimbo na kikabila, bali watoke kimasomaso kujenga na kushikamana kwa pamoja kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Nigeria. Udini, ukabila na umajimbo hauna mashiko wala mvuto kwa ustawi na maendeleo ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.