2016-02-24 15:11:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya III ya Kwaresima


“Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau lakini mimi sitakusahau kamwe” (Is 49:15). Kifungu hiki cha Biblia kinafungua tafakari yetu ya Dominika hii ya tatu ya Kwaresima ambapo tunatakafari kwa karibu zaidi tabia ya huruma ya Mungu na kile kinachotarajiwa kutoka kwetu tunapoihitaji huruma yake.

Katika Somo la Kwanza Mungu anajifunua kwa Musa na kuonesha nia yake ya kutaka kulikomboa taifa lake teule la Israeli. Hapa anaithibitisha ahadi yake kwa Babu wetu wa imani Ibrahimu kwamba atauzidisha uzao wake kama nyota za mbinguni au kama mchanga wa Pwani. Taifa hili lipo katika hatari ya kuangamizwa. Farao mfalme wa Misri amedhamiria kabisa kuwaangamiza ili kuwapunguza nguvu na hivyo wanaingia katika hali ya utumwa. Wao waliiacha nchi ya ahadi ambayo Mungu aliwapatia kupitia Ibrahimu na kwenda kufurahia mapochopocho ya nchi ya Misri ambayo yaliwaingiza katika utumwa. Waliamua wenyewe kutoka katika uhuru na kuwa watumwa. Hii ndiyo namna ambayo tunakuwa nayo sisi wanadamu pale tunapomwacha mwenyezi Mungu na kuishi katika hali ya uhuru bandia unaotuingiza katika hali ya utumwa wa dhambi na kuwa watumwa wa mali za kidunia, madaraka na umaarufu. Lakini tunapoanza kuhangaika na kutaabika huruma ya Mungu daima hutujia na kututoa katika utumwa huu.

Wimbo wa Zaburi umetupatia picha halisi ya huruma hiyo ya Mungu. Neno la Mungu linatuambia kwamba: “ Bwana amejaa huruma na neema, haoni hasira upesi ni mwingi wa fadhili”. Hii inamaanisha kwamba jicho lake kwetu daima limejaa huruma. Sisi wanadamu hata tunapoangukia dhambini bado hatuachi, anatukimbilia ili kutuokoa. Matendo yake haya makuu yameonekana tangu mwanzoni kabisa mwa historia ya wokovu wetu alipomwambia shetani “nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke,  na kati ya uzao wako na uzao wake” (Mw 3:15). Mwenyezi Mungu anaendelea kumtazama mwanadamu katika jicho lake la huruma kwani anajua kwa hakika kwamba alimuumba vema. Yeye anatafuta kutoa katika njia mbaya aliyojichagulia ili apate kuishi katika yeye. Yeye mwenyewe anasema kwa kinywa cha nabii Ezekieli kwamba “sikufurahii kufa kwake afaye, Basi ghairini mkaishi” (Ez 18:32).

Mungu wetu katika huruma yake kwetu anatualika daima kujitafakari njia zetu na kutubu. Bila utayari wetu katika kufanya toba tutaangamia. Somo la Injili linatuwekea wazi onyo hilo kwamba “msipotubu, ninyi nyote mtaangamia”. Ni onyo kwetu kwamba katika kuikimbilia hii huruma ya Mungu hakuna njia ya mkato. Ni lazima kupitia njia ya toba. Hili ndilo tunaloalikwa katika kipindi hiki cha Kwaresima. Zaidi ya hapo Mwenyezi Mungu anaonesha jinsi ambavyo anaendelea kututukuza na kuithamini nafasi yetu katika uhuru wa utashi wetu. Kwa hakika yeye hakifurahii kifo chetu, yaani kuingia kwetu katika hali ya dhambi na ndiyo maana anatafuta kila njia na anakuwa wa kwanza kutujia na kuanzisha safari ya wokovu ndani mwetu. Lakini Yeye haondoi uhuru wetu. Anachofanya Yeye ni kutuangazia na kutuonyesha njia na pale tutakapoiona lakini tukaacha kuifuata hakika tutaangamia.

Kanisa ni chombo mahsusi kilichowekwa na Bwana wetu Yesu Kristo kusudi tupate kuiona njia. Kupitia matukio na nafasi mbalimbali tunaelekezwa katika kuiona huruma ya Mungu na kuikimbilia kwa ajili ya wokovu. Kanisa linaendelea kutuombea kwa Mungu kila mara likisema: “Bwana uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; na ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate”. Ni utetezi wa hali ya juu kabisa tunaofanyiwa na Mama Kanisa kwa kuendelea kuiomba huruma ya Mungu. Mwaka huu kwa namna ya pekee tumepewa nafasi katika Jubilei ya Huruma ya Mungu, nafasi ambayo inalipatia Kanisa muda wa kupalilia kupitia Neno lake na kutilia samadi kwa Sakramenti zake. Wakrsito wenzako na wanadamu wenzako wanaendelea kukulilia mbele ya Mungu kwa ajili ya wokovu wako.

Katika hili pia twapaswa kujiadhari na kasumba inayoendelea kusambaa vichwani mwa baadhi wanaopenda njia rahisi. Leo hii inaposisitiziwa ndani ya Kanisa dhana ya huruma basi upo upotoshaji unaoenea kwamba huruma na msamaha huo upo bwerere tu bila tendo la toba. Hili ni kutaka kumgeuza mwanadamu kuwa kama mashine ambayo daima inatii amri ya anayeiendesha na kwa upande mwingine ni kumgeuza Mungu kama dikteta ambaye anaamrisha tu na mwanadamu lazima aendane na amri zake. Huu ni uposhwaji na udhalilishaji wa hadhi ya mwanadamu na asili ya upendo wa Mungu. Wokovu wetu unahitaji utayari wetu na huruma ya Mungu inatenda kazi ndani mwetu pale tu tunakuwa tayari na kujiweka katika hali ya toba.

“Macho yangu humwelekea Bwana daima, naye atanitoa miguu yangu katika wavu”. Mwaliko huu kutoka antifona ya mwanzao ya Dominika ya leo unatupatia njia ya kupitia kuikimbilia huruma ya Mungu. Mwaliko huu unatutaka daima kumwelekea Bwana. Huku ndiko kuambatana naye huku ukiwa na matumaini ya ulinzi wake na msaada wake katika kupambana na changamoto mbalimbali za ulimwengu huu. Mtume Paulo katika somo la pili anatuambia kwamba tusifikiri kukaa ndani ya maji basi ndiyo tumetakata. Tunaweza kugeuka kama jiwe mtoni ambalo maji hulipitia daima lakini ukilipasua ndani ni kavu kabisa. Tunakumbushwa kwamba “tusiache mbachao kwa msala upitao”. Ulimwengu huu unaweza kutusonga na kusahau kunufaika kwa nafasi mbalimbali za neema zinaletwa kwetu na Mama Kanisa. Nakualika leo hii kusimama na kuitambua nafasi hii ya neema inayokujia kwa njia ya huduma za Kanisa. Tuichangamkie fursa hii ili atakapokuja Bwana asitukatilie mbali bali afurahie matunda tutakayoyazaa kwa maisha yetu mema ya ushuhuda wa Injili.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.