2016-02-24 14:11:00

Miaka 25 ya huduma Radio Vatican!


Padre Federico Lombardi, SJ., baada ya kuitumikia Radio Vatican kwa kipindi cha miaka 25 anang’atuka kutoka madarakani, baada ya kuanza utume wake kama Mkurugenzi wa Vipindi kunako mwaka 1990; mwaka 2005 akateuliwa kuwa Mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican. Kunako mwaka 2001 alikabidhiwa Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV kukisimamia na mwaka 2006 akateuliwa kuwa ni Msemaji mkuu wa Vatican, huduma ambayo bado anaendelea kuifanya kwa dhamana ya Baba Mtakatifu Francisko.

Padre Lombardi anakiri kwamba, alipoteuliwa na wakuu wake wa Shirika kufanya utume wake Radio Vatican, alipata uzoefu kidogo kama Mkurugenzi wa Jarida la “Civiltà Cattolica” linalosimamiwa na kuratibiwa na Wayesuit, utume ambao aliutekeleza kwa kipindi cha miaka 10. Huu ukawa ni mwanzo wa msingi katika ulimwengu wa mawasiliano sanjari na huduma kwa Mapapa na Vatican katika ujumla wake. Aliguswa na kuvutwa kwa namna ya pekee na mwelekeo mpana wa shughuli za upashanaji habari zilizokuwa zinatekelezwa na Radio Vatican sehemu mbali mbali za dunia.

Hii ilikuwa ni Jumuiya ya Kimataifa iliyokuwa inaundwa na wafanyakazi kutoka katika mataifa 60 wenye tamaduni, lugha na mapokeo yanayotofautiana kabisa. Padre Lombardi ambaye kitaaluma ni mwanahesabu, akajifunza kuandika kwa ufupi na kwa kipindi cha miaka 15 kama Mkurugenzi wa Vipindi, yaani kuanzia mwaka 2005, akajielekeza zaidi katika kuangalia maudhui ya habari zilizokuwa zinatolewa na Radio Vatican. Akawa karibu sana na wafanyakazi katika kuandaa na kutangaza vipindi mbali mbali.

Padre Lombardi anakiri kwamba, hiki ni kati ya vipindi muhimu sana katika historia ya maisha yake; muda ambo alifurahia kukaa na kufanya kazi na watu; akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume wake kwa Radio Vatican. Radio ikawa ni Altare ya sadaka ya maisha yake ya kila siku pasi na ukomo! Kunako mwaka 2001 akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV na kunako mwaka 2006 akateuliwa kuwa ni Msemaji mkuu wa Vatican. Kazi zote hizi mbili hazikuwa na mgogoro, lakini ilimbidi kuratibu muda wake ili kuweza kutekeleza majukumu yote haya kwa kiwango na ubora unaotakiwa. Lakini, Radio Vatican iliendelea kuwa ni nyumbani kwake, huduma aliyotoa kwa moyo na akili yake yote pasi na kujibakiza.

Padre Lombardi anasema, penye urembo hapakosi urimbo. Anakumbuka shutuma zilizotolewa dhidi ya Radio Vatican kunako mwaka 2001 kwamba, mitambo yake ilikuwa inasababisha saratani na hivyo kupelekea vifo vya watoto wadogo, shutuma ambazo hazikuwa na ukweli ndani yake. Lakini, uongozi wa Radio Vatican uliendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuwajibika, kwa uvumilivu na utulivu wa kimaadili uliojikita katika ushahidi wa kisayansi. Lakini anafurahia kusema kwamba, alikuwa anapata faraja kubwa moyoni mwake kwa kupokea barua na shukrani kutoka kwa wasikilizaji wa Radio Vatican waliokuwa wanaishi katika maeneo tete yenye vita na mipasuko ya kijamii.

Kwa masikitiko makubwa, anakiri kwamba, hakuweza kuanzisha Programu kwa lugha ya Kihausa kutoka Nigeria, lugha inayotumiwa na watu wengi huko Nigeria, hususan katika eneo ambalo kwa wakati huu limekuwa ni maskani ya Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram. Hii ni huduma ambayo ingeweza kutolewa kwa gharama kidogo kabisa lakini kwa mafao ya wasikilizaji wengi nchini Nigeria. Ni huduma ambayo inaweza kuanzishwa na kuendelezwa kwa ushirikiano kati ya Radio Vatican na Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria.

Radio Vatican katika kipindi cha miaka 85 ya uwepo na huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Kanisa na Jamii katika ujumla wake, imefanya mengi ambayo yataendelea kukumbukwa katika historia. Kwa sasa kuna changamoto kubwa, kumbe hata rasilimali watu na fedha hazina budi kuelekezwa vyema. Radio Vatican imekuwa ni sauti ya kinabii kwa wanyonge na katika nchi zile ambazo zilikuwa zinatawaliwa kwa mabavu sanjari na Kanisa kunyanyasika.

Radio Vatican ikaibuka kidedea na kukonga nyoyo za watu wengi waliopata faraja na huruma kwa kusikiliza vipindi na matangazo yake. Maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, wakaona mwanga na matumaini ya maisha mapya katika mchakato wa kukabiliana na changamoto za maisha! Mageuzi makubwa yanayoendelea kutekelezwa kwenye vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican ni muhimu sana kwa kusoma alama za nyakati, ili kwenda sanjari na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya habari katika ulimwengu wa utandawazi.

Tangu mwaka 2006 kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika matumizi ya sayansi na teknolojia kwa Radio Vatican. Leo hii Radio Vatican inarusha matangazo yake kwa njia ya sauti, watu wanaweza kusoma taarifa mbali mbali kutoka kwenye mtandao wake, wanaweza kuangalia picha na kufuatilia matukio mbali mbali kwa njia ya video. Leo hii Radio Vatican ina mwelekeo mpya zaidi, ikilinganishwa na mtazamo wa radio za kawaida na si kweli kwamba Radio ina mwelekeo finyu kama baadhi ya watu wanataka kuaminishwa, ili kubana matumizi. Mtandao wa Radio Vatican ni ushuhuda makini wa huduma inayotolewa kwa wasikiliaji, wasomaji na watazamaji wake.

Padre Lombardi anasema, mageuzi ni muhimu, lakini hayana budi kuzingatia historia ya vyombo vya mawasiliano ya Vatican na kwamba, kuunganisha Radio Vatican na Kituo cha Televisheni cha Vatican si jambo geni kwani taasisi hizi mbili zimekuwa zikifanya kazi kwa pamoja. Radio Vatican ikitoa sauti na picha kutolewa na Kituo cha Televisheni cha Vatican. Mchakato wa kubana matumizi hauna budi kuzingatia ubora na wingi wa huduma inayotolewa. Radio Vatican imekuwa ni chombo kikuu cha huduma ndani na nje ya Vatican. Hapa watu wameweza kupata nyaraka za Kanisa na Makanisa mahalia, kumbe, kuna haja ya kuendelea kuwekeza kwa rasilimali watu na teknolojia ili kupata ufanisi zaidi.

Padre Lombardi anakaza kusema, hazina kubwa ya Radio Vatican inajikita katika utamaduni na rasilimali watu, ambao wamejisadaka kwa ajili ya huduma ya Kanisa kwa kuwa na matangazo kwa zaidi ya lugha 40. Huu ni mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano unaojionesha pia katika utofauti wake ambao ni hazina na utajiri mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa. Umoja unafumbatwa katika utume wa Kanisa; utofauti unajionesha katika lugha. Radio Vatican ni shule ya Ukatoliki wa Kanisa, hazina ambayo inapaswa kukuzwa na kudumishwa. Kuanzishwa kwa matangazo kwa lugha ya Kikorea ni ushuhuda wa ushirikiano kati ya Radio Vatican, Ubalozi wa Korea na Baraza la Maaskofu Katoliki Korea. Kwa mtazamo huu, Radio Vatican inaweza kuendelea kupanua wigo wake zaidi kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu.

Radio Vatican ni hija ya wongofu wa ndani unaojikita katika changamani za maisha ya watu na teknolojia. Kutoka katika matangazo ya Radio kwa njia ya analogia hadi kuingia mtindo wa digitali, hapa si haba yataka moyo kweli kweli! Kuna wafanyakazi 300 wanaojisadaka kila siku kwenye Radio Vatican kwa kuonesha weledi na upendo wao kwa Kanisa katika huduma wanayotoa kwa Familia ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Nafasi za ajira zinapaswa kuboreshwa zaidi, ili kuwapatia wafanyakazi motisha zaidi sanjari na kufanya maboresho katika taaluma na mikataba ya wafanyakazi ambayo kwa miaka mingi imedumaa kidogo.

Huu ni mwaliko wa kufanya hija ya pamoja kwa kushikamana ili kukabiliana na changamoto mpya katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa muda wa miaka 80 viongozi wakuu wa Kanisa waliwakabidhi Wayesuit kuongoza na kuisimamia Radio Vatican, utume ambao wameutekeleza kwa ari na moyo mkuu; kwa sadaka na majitoleo pasi na kutafuta makuu. Wamesaidia kupunguza gharama za uendeshaji kwani wao kama watawa, walikuwa wanalipwa “kiduchu”. Wamekumbana na mashaka, lakini wakawa na ujasiri wa kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa. Wayesuit wameshirikiana kwa hali na mali na wafanyakazi wote wa Radio Vatican.

Padre Lombardi anasema, Baba Mtakatifu Francisko amewaomba Wayesuit kukaa pembeni kidogo na Radio Vatican ili kuendeleza utume wao katika nyanja nyingine za mawasiliano. Padre Federico Lombardi, SJ., anakuwa ni mkurugenzi wa mwisho wa Radio Vatican kutoka katika Shirika la Wayesuit. Ni matumaini yake kwamba, Sektrtarieti ya Vatican itaendeleza majadiliano na viongozi wa Shirika la Wayesuit kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Radio Vatican. Kwa sasa wataendelea kushirikiana na wafanyakazi wengine wa Radio Vatican pamoja na kusimamia vipindi vya Radio Vatican, ili mchakato wa mageuzi uweze kuleta matunda yanayokusudiwa. Wote kwa pamoja hawana budi kusonga mbele kwa imani na matumaini sanjari na kutekeleza vyema wajibu na dhamana iliyoko mbele yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.