2016-02-24 08:50:00

Kushukuru ni kuomba tena!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya hivi karibuni limeadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kufanikisha hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Kenya kuanzia tarehe 25- 27 Novemba 2015. Ibada hii imeongozwa na Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi na kuhudhuriwa na Maaskofu, Wakleri, Watawa na Waamini walei pamoja na wawakilishi wa viongozi wa Serikali nchini Kenya.

Askofu Peter Kihara wa Jimbo Katoliki la Marsabit, Kenya katika mahubiri yake amesema kwamba, hija ya Baba Mtakatifu nchini Kenya imekuwa ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia yote ya Mungu nchini Kenya. Watu wengi wamevutwa na kuguswa na mahubiri pamoja na hotuba za Baba Mtakatifu Francisko zilizogusa kwa undani matatizo, changamoto na matumaini ya familia ya Mungu nchini Kenya. Baba Mtakatifu katika hija yake ya kitume nchini Kenya, aliwataka wakenya kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Wananchi wa Kenya wanapaswa kuondokana na misimamo mikali ya kidini ambayo haina mvuto wala mashiko; kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote sanjari na kusimama kidete kupambana na umaskini, rushwa, ufisadi, udini na ukabila; daima mwanadamu na mahitaji yake msingi akipewa kipaumbele cha kwanza. Yote haya ni tisa, kumi ni ushuhuda wa maisha na unyenyekevu wa Baba Mtakatifu Francisko umekuwa na mvuto mkubwa kwa wananchi wengi wa Kenya! Kwa hakika wamemwona kuwa ni mtu wa watu kwa ajili ya watu!

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuweza kufuata na kutekeleza ratiba ngumu iliyokuwa mbele yake wakati wa hija yake ya kitume nchini Kenya, licha ya umri wake. Wanamshukuru kwa kuamua kutembelea Kenya ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo. Mahubiri na ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Kenya kwa sasa umewekwa kwenye vitabu na DVD tayari kuwasaidia wananchi kufanya rejea kwa tukio hili la kihistoria nchini Kenya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CISA.








All the contents on this site are copyrighted ©.