2016-02-23 09:20:00

Padre Federico Lombardi astaafu rasmi


Mwishoni mwa Februari 2016, Viongozi Wakuu wawili mashuhuri Radio Vatican,  wanag'atuka rasmi. Wahusika ni Padre Federico Lombardi, Mkurugenzi wa  Radio Vatican,  na Alberto Gasbarri Mkurugenzi wa Utawala wa Radio, ambaye pia alikuwa ni mratibu wa ziara za Kipapa. Padre  Federico Lombardi SJ, anang’atuka baada ya kuitumikia "Radio ya Papa"kwa muda wa miaka 26. Alianza utume huo kama Mkurugenzi wa Mipango  na mwaka 2005, akawa  Mkurugenzi Mkuu. Hata hivyo , anaendelea kulitumikia kanisa kama  Mkurugenzi wa Ofisi ya Habari ya Jimbo Takatifu .

Katika kipindi hiki, kuna mabadiliko mengi yanayofanywa ndani ya Redio Vatican , "Radio ya Papa" , kama ilivyoamuliwa na Sekretariat  ya Mwasiliano iliyoundwa na Papa Francisko mwezi June ,kwa ajili ya kufanya mabadiliko katika sekta nzima ya Mawasiliano Vatican.Lengo ni  kupunguza gharama za uendeshaji za Idara hiyo, inayotajwa kutumia sehemu kubwa ya fedha katika bajeti ya Vatican. Aidha Mkurugenzi wa Ofisi Radio Vatican, Dr. Alberto Gasbarri, kwa  karibia kipindi cha miaka 40  iliyopita, amekuwa akiratibu ziara za Kipapa, naye pia anastaafu kwa mujibu wa umri.

Wakati huo huo, bila ya kutangaza watakaochukua nafasi ya Padre  Lombardi au ile ya  Gasbarri , Padre  Dario Edoardo Viganò, Mkuu wa Sekretarieti ya Vatican kwa ajili ya Mawasiliano , ametangaza kuteuliwa kwa muda , Mlei Mwanasheria, Wakili Giacomo Ghisani, kuwa kiongozi wa muda wa Radio Vatican, na pia kama  Mwakilishi wa kisheria na Mkurugenzi wa Utawala Redio Vatican.  Hadi uteuzi mpya  Ghisani, alikuwa akitumikia Radio Vatican kama Mkuu wa Uhusiano wa Kimataifa na Mambo ya Kisheria kwa Radio Vatican, pia kama  Makamu wa Mkurugenzi wa Sekretarieti ya Mawasiliano.

Padre  Viganò katika tamko lake juu ya  kuteuliwa kwa  Ghisani,amesema ameteuliwa kulingana na mazingira ya  maamuzi ya kuwa na mchakato wa kufanya mapitio  na marekebisho kwa ajili ya  kuunganisha vyombo vya  habari vya Vatican , sambamba na Barua binafsi ya Papa Francisko “Motu proprio" iliyoanzisha Sekretarieti ya Mawasiliano hapo  tarehe 27 Juni 2015 ambayo inaendelea kufanya kazi hizo. "Motu proprio"  ya Papa ilitaka vyombo vya  mawasiliano vyote vya Vatican viunganishwe  chini ya idara moja mpya, badala ya kila idara kujitegemea. Idara husika zinazounganishwa ni pamoja na  Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mawasiliano ya Jamii, Ofisi ya kupiga chapa,Huduma ya Internet , Radio,  Kituo cha Televisheni, Gazeti la Osservatore Romano, Ofisi ya habari na  Huduma  ya Picha.

Mpaka sasa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mawasiliano ya Jamii na Ofisi ya Habari ya Jimbo Takatifu, tayari zimeungana katika hatua za kiutawala na usimamizi wa shughuli.  Aidha Radio na  kituo cha Televisheni , kiutawala zimeunganishwa na zinashirikishana rasilimali kwa ajili ya utoaji wa huduma kwa pamoja.  Tamko la Sekretariat  pia linasema, kazi kubwa iliyoko mbele yao ni kuongeza ubora katika huduma, ikiwa ni pamoja na urithi wa lugha na tamaduni mbalimbali zinazokutanishwa katika hali halisi ya shughuli za vyombo vya Mawasiliano Vatican. Kwa mujibu wa Taarifa , kwa wakati huu  Mkurugenzi wa sasa wa Matangazo wa Radio Vatican, Padre  Andrzej Majewski SJ, ataendelea kuwa msimamizi wa kazi  ya wahariri na waandishi wa habari na Sandro Piervenanzi itaendelea kusimamia masuala ya teknolojia ya Radio.








All the contents on this site are copyrighted ©.