2016-02-23 14:50:00

Mwaka wa Huruma ya Mungu Jimbo kuu Dodoma


Nianze kwa kuwatakieni nyote Baraka nyingi kwa kipndi hiki cha kwaresma ni kipindi ambacho mwenyizi mungu anatupatia Baraka nyingi sana mradi tu tukitumie vizuri .tunakitumiaaje vizuri: kwa kusafiri kiroho pamoja na bwana watu yesu kristu ambaye kwa mateso kifo na ufufuko wake, ameipatia dunia wokovu. Safari hii inakuwa pia ni maandalizi kwa kupata maisha ya milele mbinguni pamoja na Baba.  Pili kwa kukiri kuwa sisi ni wadhambi na kwamba, tunahitaji kufanya toba na kupata msamaha wa madhambi yetu. Tatu, kwa kusali zaidi ikiwa ni pamoja na kusali njia ya Msalaba na kurudi katika Sakramenti mbalimbali hasa kwa wale waliojisahau. Nne, kwa kujisadaka , kufunga n a kutoa sadaka kwa wanaohitaji zaidi.

Wapendwa

Tukichunguza kwa umakini hayo mambo manne hapo juu , tunona kuwa karibu yote yanafanana na ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kwa kifupi ni kwamba Baba Mtakatifu ametangaza mwaka huu wa 2016 uwe Mwaka wa huruma ya Mungu, lengo ni kutoa fursa kwa waamini wote duniani kutafakari kwa ukaribu zaidi msamaha, huruma , na ukarimu wa Mwenyezi Mungu usio na mipaka. Kukutana na huruma ya Mungu maana yake kukutana na Mungu kukutana huku na mungu kwa ukaribu zaidi kutatusukuma kubadili namna yetu ya kuishi, namna yetu ya kuhusiana na wengine pia mtazamo wetu wa maisha kwa ujumla. Nawalikeni kwanza kabisa tusali ili tunapoadhimisha kwaresma hii na mwaka huu wa huruma ya Mungu mioyo yetu iguswe kwa namna ya pekee na tubadilike .

Nawalikeni kuchunguza hali yetu ya kiroho, baadhi yetu hatupokei Sakramenti mbalimbali kwa muda mrefu nawahimiza kutumia kipindi cha hiki kupata sakramenti hizo tuwe na tabia ya kupata Sakramenti hii ya mara kwa mara. Moja ya eneo ambalo lazima litazamwe kwa karibu na Sakramenti ya ndoa, wengine tunaishi unyumba [kama mme na mke ] bila Sakrameti ya ndoa katika Mwaka huu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, nawaalika wote wenye shida ya namna hii wajiandikishe kwa maparoko. Nawaagiza maparoko wote wa tangaze tarehe ya kuanza semina ya ndoa kwa watu wote wanaoishi bila ndoa,waeleze semina hii itaanza lini na siku ambayo ndoa zote zitabarikiwa.

Hii itasaidia sana wale wanaoacha kubariki ndoa zao kwa kisingizio eti na gharama kubwa, narudi kwa Mwaka huu ndoa zote zitayarishwe kwa pamoja na kubarikwa siku moja. Baada ya ibada Paroko awakusanye waliobariki ndoa na kuwapongeza. Baada ya hapo kila mmoja aende nyumbani kwake kwa amani. Nichukue nafasi hii kuwakumbusha wote kuwa ndoa ni Sakramenti na sio sherehe. Ni matarajio yangu kwamba tutakapomaliza mwaka huu wa HURUMA YA MUNGU Siku kuu ya Kristo mfalme, hakutakuwepo tena Mkristo ambaye bado atakuwa anaishi bila Sakramenti ya ndoa.

Eneo jingine ambalo nalo linahitaji Huruma ya mungu ni ubatizo wa watoto wadogo. Tunao utaratibu wa kutowabatiza kwa urahisi watoto waliozaliwa nje ya ndoa. Lengo sio kuwaadhibu watoto, bali ni kuwasaidia wazazi au mama aliyezaa nje ya ndoa aingie katika maisha salama ya ndoa. Najua wapo watoto wengi wa aina hiyo ambao wamenyimwa ubatizo. Wengine hawajabatizwa kwa sababu ya uvivu wa wazazi kuwaleta Kanisani. Kwa kuwa ni mwaka wa HURUMA YA MUNGU, naagiza Maparoko wote kuwafungulia wote waliozuiliwa kwa sababu yoyote ile. Maparoko na mapadre wote hakikisheni mwaka huu watoto wote wanabatizwa bila ya masharti yoyote, mradi tu wahusika wawe tayari kuhudhuria semina ya matayarisho ya ubatizo wa mtoto.

Sakramenti ya Upatanisho nayo inahitaji kutazamwa kwa ndani. Ni tabia nzuri kupenda kuomba toba na msamaha kwa Mungu tunapoanguka katika dhambi. Tupende kupata sakramenti ya kitubio mara kwa mara, Sakramenti ambayo inatuonjesha huruma ya Mungu kwa ukaribu kabisa, Mungu asiyependa kuadhibu bali kusamehe. Tukumbuke kuwa hakuna dhambi isiyosamehewa na Mungu isipokuwa ile ya kukata tamaa na kusema “ Mungu hatanisamehe, ndio kumkufuru Roho mtakatifu”.

REHEMA KAMILI.

Wapendwa,

Kama ilivyo katika mwaka wowote wa jubilei , mwaka huu wa HURUMA YA MUNGU, REHEMA KAMILI itatolewa vilevile. Kazi ya rehema kamili ni kuondoa makovu yatokanayo na dhambi. Tukumbuke kwamba dhambi ni kukata tamaa kwa jinsi Mungu anavyotaka tuwe – ni kumkataa Mungu. Tunapoungama, dhambi zetu zinasafishwa lakini kovu lililosababishwa linabaki kama ilivyo kawaida kwa kidonda kuacha kovu. Kovu hili ambalo hubaki hata baada ya kupata maondoleo ya dhambi huondolewa kwa namna mbili. Au kwa kupitia toharani baada ya kifo, au kwa kupata rehema kamili tukiwa bado hapa duniani. Rehema kamili kijumla ilitolewa mara ya mwisho wakati tunaadhimisha jubilee kuu ya mwaka 2000.

Masharti ya kupata rehema kamili ni haya yafuatayo:

1. Lazima uungame dhambi zako

2. Halafu upokee Sakramenti ya Ekarist Takatifu

3. Ufanye hija mahali palipoteuliwa rasmi na Askofu ( kwa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma maeneo yaliyoteuliwa ni haya yafuatayo: Kanisa kuu , Podium Mbwanga- miyuji( Kituo cha kiroho cha Askofu Mathias Issuja ) na Kanisa la Mpwapwa.

4. Usali baba yetu moja, salamu maria moja, atukuzwe baba moja kwa nia za Papa.

 

MATENDO YA HURUMA: KIROHO NA KIMWILI.

Jambo jingine ambalo tunatarajiwa kufanya katika kipindi hiki cha mwaka wa HURUMA YA MUNGU na ambalo Mama Kanisa analihimiza san katika kipindi hiki cha kwaresma ni kuwafikiria , kuwatembelea na kuwasaidia kwa karibu zaidi wale walio katika dhiki kuliko sisi wenyewe.

Nawahimiza kupenda kufanya yafuatayo:

1. Kuwasaidia wenye njaa na wasio na nguo kama una ziada kidogo

2. Kuwatembelea wagonjwa majumbani na mahospitalini

3. Kuwashauri walegevu warudi katika Sakramenti

4. Kusamehe waliotukosea kama Mwenyezi Mungu anavyotusamehe sisi makosa yetu.

5. Kuwafariji walio katika matatizo ya kimaisha kwa kuwapa ushauri mzuri

6. Kuwaombea marehemu

7. Kusali kwa ajili ya Amani na maendeleo ya familia zetu na Taifa letu.

KUFUNGA: Nipende kumalizia ujumbe huu kwa kuwakumbusha utamaduni wa muda mrefu wa kufunga kipindi hiki cha KWARESMA . Wanaostahili kufunga ni wale walio na umri wa miaka 18 hadi 59. Lakini mmoja mwenye shida ya afya hatakiwi kufunga. kufunga maana yake kupata mlo mmoja kamili na mingine iwe miepesi. Ni wakati wa kuacha yale yote yanayotuangusha katika dhambi.

SHUKRANI: Nawashukuru madekano wote, maparoko wote, mapadre wote, watawa wote, viongozi wa halmashauri ya walei, viongozi wa aina zote na waamini wote kwa yale yote mema mlioyonifanyia mwaka uliopita wa 2015. ASANTENI SANA. Pia napenda tuwakumbushe kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa viongozi katika ngazi mbalimbali za Kanisa. Niombe tuwachague watu ambao wako tayari kumwaga jasho lao kwa maendeleo ya Kanisa. Niwahimize pia mapadre wote kuendelea kwa juhudi mpya katika kufundisha Katekesi ya kina, kutoa Sakramenti bila kujali hali, hasa kuwahudumia wagonjwa na wenye mashauri ya kiroho. Matatizo yote ya ndoa yaandikwe vizuri na kuletwa kwangu baada ya kupita kwa kamati ya usuluhishi.

NAWATAKIENI TENA NYOTE BARAKA NYINGI ZA KWARESMA, PASAKA NA MWAKA WA JUBILEI YA HURUMA YA MUNGU ULIOSHEHENI NEEMA ZA MWENYEZI MUNGU.

Mtumishi wenu mkuu,

Beatus Kinyaiya, OFMCap.

Askofu mkuu – Jimbo Kuu Katoliki Dodoma .

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.