2016-02-20 08:50:00

Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto ya kijamii!


Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira  Laudato si ni changamoto kubwa katika uwajibikaji wa kijamii ili kulinda, kutunza na kuendeleza kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa kwake na Mwenyezi Mungu. Kushindwa kutekeleza dhamana hii ni kutaka kuwatumbukiza watu katika maafa na majanga ya maisha na kwamba, waathirika wakuu ni maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hapa, Jumuiya ya Kimataifa inachangamotishwa kuona na kuhisi athari za mabadiliko ya tabianchi katika maisha ya kila siku tayari kuambata sera makini za utunzaji bora wa mazingira. Wongofu wa kiekolojia ni dhamana nyeti inayopaswa kufanyiwa kazi na wengi ili kutunza mazingira na kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa za kijamii.

Haya ni kati ya mambo muhimu yaliyopewa kipaumbele cha pekee hivi karibuni na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani wakati akitoa mhadhara kwa washiriki wa Mkutano wa Kimataifa kuhsu utunzaji bora wa mazingira na Jamii kwenye Jumuiya ya Chuo kikuu cha St. Thomas, kilichoko Miami, nchini Marekani. Wajumbe wamepata nafasi ya kusikiliza kwa kina na mapana kuhusu mazingira asilia, jamii, uchumi na siasa changamani. Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha watu kutoa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira; kwa kujikita katika majadiliano yanayofumbata wongofu wa kiekolojia; elimu makini ya uraia na utunzaji bora wa mazingira; kanuni maadili na utu wema sanjari na kujikita katika uelewa mpana wa changamoto hizi katika maisha ya kiroho, ili kuchukua hatua muhimu katika utunzaji bora wa mazingira, kwa kutambua kwamba, mambo haya yanaathari katika maisha ya kijamii.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukabiliana na changamoto hizi kwa kuzama zaidi katika imani, utu na heshima yao; kwa kushirikiana na kushikamana ili kulinda na kudumisha mazingira, nyumba ya wote. Ili kufanikisha, yote haya kuna haja ya kukazia katika wongofu unaojikita katika maisha ya mtu binafsi, makundi na taasisi katika ngazi mbali mbali za maisha; kwa watu mahalia sanjari na Jumuiya ya Kimataifa. Kardinali Turkson amewafafanulia Waraka huu ambao kwa sasa umekuwa kama ni sehemu ya utambulisho wake sehemu mbali mbali za dunia; tayari kwa wananchi katika maeneo yao pia kufanya maamuzi machungu, ili kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira, nyumba ya wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.