2016-02-20 08:01:00

Ni hija ya huruma ya Mungu inayofumbatwa katika amani na matumaini!


Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Radio Vatican amefanya rejea kwa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Mexico kuanzia tarehe 12 hadi 18 Februari 2016, iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Papa Francisko mmissionari wa huruma ya Mungu na mjumbe wa amani. Anasema, mafundisho makuu ya Baba Mtakatifu kwa wakati huu ni kuendelea kuhamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu; kwa kuwa na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu; upendo, haki, amani na upatanisho.

Ni mwaliko wa kuonesha mshikamano na maskini, wakimbizi na wahamiaji pamoja na wote wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Changamoto hii si kwa ajili ya kumshambulia mtu awaye yote, kama ambavyo imechukuliwa na vyombo vingi vya habari kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amemshambulia kwa maneno Bwana Donald Trump, moja ya wagombea Urais nchini Marekani. Baba Mtakatifu hapendi kuingilia mambo ya kampeni za kisiasa, bali anapenda kukazia kwa namna ya pekee sera na mikakati inayojikita katika huruma, upendo na mshikamano kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; mambo yanayoweza kufanikishwa kwa kujenga na kudumisha madaraja yanayowakutanisha watu! Huu ndio mwelekeo sahihi kutoka kwa Baba Mtakatifu kuhusiana na kampeni za kisiasa zinazofanywa na Bwana Donald Trump, huko Marekani.

Padre Lombardi anaendelea kufafanua kamba, Baba Mtakatifu amegusia kwa kina na mapana kuhusu Tamko la kichungaji lililotolewa kati yake na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima. Ameonesha uhusiano wake wa karibu na Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk wa Kanisa la Kigiriki la Kikatoliki kutoka Ukraine, aliyezungumzia kuhusu tukio hili la kihistoria na matokeo yake katika maisha na utume wa Makanisa haya mawili na hatimaye, kuonesha mawazo yake binafsi kuhusu Tamko hili la kichungaji, chachu ya ushirikiano kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox la Russia.

Baadhi ya viongozi wa Kanisa kutoka Ukraine hawakupokea kwa mikono miwili yale yaliyoandikwa kwenye Tamko hili. Hapa Padre Lombardi anafafanua kwamba Tamko hili linajikita katika matumaini ya amani, dhamana na wajibu wa kutafuta na kudumisha amani na kwamba, Mkataba wa Amani wa Minsk unapaswa kuheshimiwa na kutekelezwa, ili kweli amani na utulivu viweze kurejeshwa tena nchini Ukraine. Maisha na utume wa Kanisa la Kigiriki la Kikatoliki umejadiliwa kwa mapana katika Tamko hili. Baba Mtakatifu anafahamu matatizo na changamoto zinazowakabili waamini huko Ukraine na anapenda kuwasaidia watu kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa mambo.

Kuhusu ugonjwa wa Zika, Baba Mtakatifu amekuwa mkweli na muwazi kwamba, utamaduni wa kifo unaotaka kuhalalisha utoaji mimba kama sehemu ya mchakato wa kupambana na Virusi hivi, haukubaliki na kwamba, watu wawe makini na kama kuna dharura, hatua makini zinaweza kuchukuliwa. Ni mwelekeo kama huu ulikwisha wahi kutolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika mahojiano kwenye kitabu cha “Luce del Mondo” kuhusu matumizi ya Kondom kama kinga dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi.

Hapa alikazia umuhimu wa kuwa na dhamiri nyofu iliyofundwa na kufundika katika Mafundisho ya Kanisa. Tafiti za kisayansi, chanjo na tiba zinapaswa kuendelezwa ili kudumisha uhai wa binadamu badala ya kukimbilia njia za mkato ambazo mara nyingi zinakumbatia utamaduni wa kifo. Hata katika maamuzi yanayofanywa na wabunge katika medani mbali mbali za maisha yanapaswa kuongozwa na dhamiri nyofu; tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu, familia na jamii.Hizi ni tunu ambazo zinapaswa kulindwa na kutetewa kisheria badala ya kutumbukia katika mwono finyu kwa ajili ya mafao ya mtu binafsi. Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yanayo dhamana ya kuwafunda waamini wao mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa ili kutetea utu na heshima ya binadamu; mafao ya wengi; haki, amani na mshikamano wa dhati.

Padre Lombardi anakaza kusema, mahojiano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na waandishi wa habari wakati akirejea kutoka Mexico yamewafanya wengi kusahau yale yaliyojiri wakati wa hija yake. Lakini, hija hii imekuwa ni tukio kubwa ambalo limeimarisha utamaduni wa watu kukutana, kupendana na kushikamana tayari kulinda na kudumisha ustawi na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu amegusa undani wa wananchi wa Mexico; ameonja shida, magumu na fursa walizo nazo kwa ajili ya ustawi wa wengi kwa kutambua kwamba, alikuwa ni Mmissionari wa huruma ya Mungu na mjumbe wa amani.

Baba Mtakatifu Francisko ameonesha Ibada yake kwa Bikira Maria wa Guadalupe, katika hali ya ukimya na majadiliano ya ndani; mambo ambayo yamegusa hija nzima ya Baba Mtakatifu huko Mexico. Papa amegusia matatizo ya: biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya na madhara yake; changamoto ya uhamiaji; magenge ya uhalifu na ukosefu wa haki msingi kwa Wahindi wekundu. Kumbe, pamoja na yote haya, Baba Mtakatifu amependa kuwatia shime na matumaini ya kusonga mbele ili kupyaisha maisha yao, tayari kukumbatia huruma ya Mungu. Ametambua uwepo wa vijana wengi nchini Mexico chachu ya matumaini, lakini wanapaswa kufundwa barabara. Padre Federico Lombardi anakaza kusema hii imekuwa ni hija ya huruma ya Mungu inayofumbatwa katika amani, matumaini na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.