2016-02-20 09:45:00

Majadiliano ya kidini ni muhimu katika kukuza na kudumisha haki na amani


Viongozi wa dini mbali mbali wanayo dhamana na wajibu wa kuhakikisha kwamba, wanasaidia kwa hali na mali mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu; kwa kuhakikisha kwamba, mafundisho msingi ya dini mbali mbali yanaeleweka vyema kwa waamini wao, tayari kuwakanya waamini wanaotumia udini kuwa chanzo cha vurugu, vita na mipasuko ya kijamii. Dini, kimsingi zimekuwa ni vyombo vya kupandikiza: haki na amani; udugu na mapendo; kwa kukuza utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Dini zimekuwa mstari wa mbele kulinda, kutetea na kudumisha tunu bora za maisha ya ndoa na familia sanjari na utunzaji bora wa mazingira.

Waamini wa dini mbali mbali wakiungana, wakashikamana na kushirikiana kwa pamoja, wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika ulimwengu mamboleo na changamoto na matatizo yanayomwandama mwanadamu. Yote haya yanapaswa kufanyika kwa kuzingatia majadiliano yanayofanyika katika ukweli na uwazi; ili kusikiliza, kufahamu na kutenda kwa ajili ya kutafuta na kudumisha mafao ya wengi. Hii ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini wakati alipokuwa anashiriki katika mkutano wa kumi na mbili wa Majadiliano ya kidini, uliokuwa unafanyika huko Doha, Qatar kwa kuongozwa na kauli mbiu “Usalama wa kiroho na kiakili katika mwanga wa Mafundisho ya Dini”. Anakaza kusema, majadiliano ya kidini ni changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo na maisha ya hadhara.

Leo hii, kuna machapisho mengi ya masuala ya kidini, lakini kwa upande mwingine, dini zinaogopesha kutokana na ukweli kwamba, kuna baadhi ya waamini wamekuwa na misimamo mikali ya kiimani kiasi hata cha kutumia dini kuhalalisha vitendo vya kigaidi na mipasuko ya kijamii. Mkutano huu ulikuwa umeandaliwa na Taasisi ya “Doha International Center for Interfaith Dialogue (DICID) iliyoanzishwa kunako mwaka 2008 na tangu wakati huo imekuwa mstari wa mbele kuitisha, kuendesha na kuratibu mikutano, makongamano na warsha kuhusiana na majadiliano ya kidini, ili kuwasaidia waamini wa dini mbali mbali kutambua na hatimaye, kuambata tunu msingi za maisha ya kidini katika maisha ya hadhara.

Kwa namna ya pekee, Taasisi hii kwa mwaka huu inapenda kujielekeza zaidi katika mchakato wa kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho, ili kukoleza misingi ya haki, amani na usalama; mambo yanayopaswa kujikita katika akili na mioyo ya watu ili kuondokana na matatizo ya maamuzi mbele, ili hatimaye, waamini wa dini mbali mbali waweze kuchangia katika usalama, ustawi na maendeleo ya nchi zao.

Huko Doha, Qatar, wajumbe wamegusia pia dhamana na wajibu wa vyombo vya mawasiliano ya kijamii katika kudhibiti dhana ya mipasuko ya kijamii na ubaguzi kwa misingi ya kidini. Inasikitisha kuona kwamba, viongozi wa kidini ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kusababisha vita, chuki na mipasuko ya kidini, ndio wanaopewa kipaumbele cha pekee na vyombo vya mawasiliano ya kijamii kama ilivyo pia kwa wanasiasa, kiasi kwamba, wanaendelea kuhatarisha amani na utulivu wa kijamii.

Wajumbe wamewataka viongozi wa kidini kuwa makini katika majiundo ya vijana: kiroho, kimaadili na kimwili, kwani kuna baadhi ya viongozi wamekuwa na mielekeo potofu kuhusu dini, mambo yanayorithishwa na kuendelezwa na vijana wa kizazi kipya. Kumbe, vijana wasaidiwe kutambua na kuheshimu tunu msingi za maisha ya kiroho; umuhimu wa majadiliano ya kidini; misingi ya haki na amani. Familia ziwe ni shule ya kwanza ya kuwafunda vijana katika maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili; ili kweli vijana waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani. Elimu dunia, itolewe vyema kwa vijana ili waweze kuandaliwa kushiriki vyema katika ustawi na maendeleo ya nchi zao, kwa kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, inayoendelea kuhatarisha amani na mafungamano ya kijamii. Kumbe, mchakato wa kutunza na kudumisha uhuru wa kiroho na kiakili ni muhimu sana katika kumwilisha tunu msingi za maisha ya kiroho ndani ya jamii.

Wajumbe wanatambua na kuthamini mchango wa majadiliano ya kidini na kwamba, majadiliano ya kidini anasema Kardinali Jean Louis Tauran hayana budi kujikita katika tunu msingi za maisha ya kijamii, haki na amani; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa kuzingatia mambo haya msingi, dini zinaweza kutoa cheche za matumaini, amani na maridhiano ndani ya jamii. Lakini, ikumbukwe kwamba, majadiliano ya kidini ni muhimu sana kwa nyakati hizi, pengine hata kuliko ilivyowahi kutokea katika historia ya binadamu huko nyuma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.