2016-02-20 06:54:00

Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wafanyakazi wa Vatican


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 22 Februari, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa ajili ya wafanyakazi wote wa Vatican. Itakumbukwa kwamba, Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, Mtume ilianza kuadhimishwa kunako karne ya nne, alama ya umoja wa Kanisa lililojengwa juu ya Mtume Petro.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wafanyakazi wote wa Vatican yaani: Wakleri, watawa na waamini walei, kwa mara ya kwanza wote watakusanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kumzungumza, Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Wafanyakazi wa Vatican katika ujumla wao ni kundi linalomsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza vyema dhamana na wajibu aliokabidhiwa na Kristo Yesu wa kuwaimarisha ndugu zake katika imani.

Jubilei ya Mwaka Mtakatifu kwa wafanyakazi wa Vatican itaanza kwa tafakari juu ya huruma ya Mungu inayopaswa kumwilishwa kila siku ya maisha; tafakari ambayo itatolewa na Padre Marko Rupnick, Myesuit anayetaka kuzama zaidi katika hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu kwa wasaidizi wake wa karibu wakati wa Siku kuu ya Noeli kama tiba muafaka ya kutibu magonjwa ya maisha ya kiroho na kitume wanayoweza kukabiliana nayo wafanyakazi wa Vatican, kwa kutambua kwamba, hata wao ni binadamu wanaweza kuelemewa na mapungufu yao ya kibinadamu. Jubilei ni fursa ya kuomba na kuambata huruma ya Mungu. Baada ya tafakari, yatafuatia maandamano makubwa kuelekea kwenye Lango la huruma ya Mungu yakiongozwa na waamini walei, watawa, mapadre na baadaye Maaskofu, Mapatriaki na Makardinali. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuanza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican majira ya saa 4:30 kwa saa za Ulaya.

Kwa waamini watakaoshiriki katika Ibada hii ya Misa Takatifu wanaweza kujipatia Rehema kamili kwa kutimiza masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa; yaani: kwa kuungama dhambi, kupokea Ekaristi Takatifu na kusali kwa ni aza Baba Mtakatifu. Haya ni masharti kwa waamini wote wanaotaka kupokea rehema kamili hata wakati wa maadhimisho katika maeneo yao. Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu kiwe ni kipindi cha toba, wongofu wa ndani na matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.