2016-02-20 14:51:00

Jubilei ya huruma ya Mungu ilete upyaisho katika maisha ya watu!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Jumamosi, tarehe 20 Februari 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, amekumbusha kwamba, Kipindi cha Kwaresima, Mama Kanisa anawaalika watoto wake  kumfahamu Kristo kwa karibu zaidi; kuishi vyema imani yao na kushuhudia huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao, kielelezo cha uwepo wao wa karibu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Haya ni mambo yanayojionesha katika upendo na huduma; katika mawazo na utekelezaji wake; ili kweli waamini hawa waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu amefafanua kwa kina na mapana dhamana ya utekelezaji na umwilishaji wa matendo ya huruma katika maisha ya kila siku, kama ushuhuda wa uaminifu, sadaka na majitoleo ya mtu. Haya ni mambo pia yanapaswa kushuhudiwa katika sala, kazi, masomo, michezo na wakati wa muda binafsi. Uwajibikaji anasema Baba Mtakatifu ni kuweka wema na nguvu zote kwa ajili ya kudumisha mchakato wa maboresho ya maisha ya watu!

Waamini wanakumbushwa kwamba, hata Mwenyezi Mungu amechukua dhamana kwa ajili ya binadamu: kwa kuumba dunia licha ya vishawishi na majaribu ya kutaka kuiharibu, lakini dhamana kubwa ni ile ya kumpatia binadamu Kristo, Mwanaye Mpendwa ili aweze kuwa kweli ni chemchemi ya yale yote ambayo mwanadamu anaomba kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Yesu ametekeleza dhamana hii kwa kuwarudishia maskini matumaini mapya ya maisha; kwa kuwapatia tena watu utu na heshima yao kama binadamu; kwa kuwahangaikia wagonjwa, wafungwa na wadhambi. Yote haya Yesu aliyafanya kwa wema na moyo mkuu, kuonesha kuwa kwa halika alikuwa ni Huruma hai ya Mungu kati ya watu waliokuwa wanateseka na kusumbuka katika maisha! Yesu aliwaendea wadhambi, akawakumbatia na kuwaonesha huruma ya Baba na kwa njia ya upendo huu, wakatubu na kumwongokea Mungu.

Hii ni changamoto kwa kila mwamini kutambua kwamba, ni mdhambi na anapaswa kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu katika hija ya maisha yake ya kiroho. Yesu ametumwa na Baba yake wa mbinguni ili kuwa karibu na binadamu, awafungulie malango ya huruma na upendo wa Mungu; tayari kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, kuiga mfano wa Kristo kwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa kutekeleza dhamana hii kikamilifu, ili kuzima kiu ya matumaini kwa wale waliokata tamaa; watu waliotengwa na kutelekezwa; wagonjwa na walemavu; wote hawa ni watu wanaohitaji kwa namna ya pekee kuonja huruma na upendo wa Mungu, ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha.

Waamini wawe kweli ni mashuhuda wa huruma ya Mungu iliyowagusa na kuwakomboa, ili kuwaonjesha wengine Injili ya furaha na matumaini. Baba Mtakatifu Francisko anatumaini kwamba, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yatasaidia akili na mioyo yao kugusa dhamana waliyokabidhiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Hii ni dhamana inayojikita katika huruma ya Mungu. Hiki kiwe ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani pamoja na kuendelea kujifunza kutoka katika shule ya Bikira Maria aliyetekeleza dhamana na wajibu wake, kwa kumtumainia Mungu, ili nao waweze kuambata utakatifu wa maisha. Waamini wawe na ujasiri wa kumwilisha ibada katika uhalisia wa maisha kama alivyowahi kusema Mtakatifu Faustina, akiwataka waamini kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu tayari kutoa msamaha kwa makosa waliyotendewa na wengine.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa watu wanaojitolea kutoa huduma kwa watu mbali mbali na kuwaambia kwamba, hiki ni kipindi cha kuvumbua tena imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Anakumbusha kwamba, tarehe 22 Februari 2016 ni Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro. Siku maalum ya umoja na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na waamini sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wafanyakazi wote wa Vatican, wanaotoa huduma kwa Watu wa Mungu kila siku ya maisha yao. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuendelea kumsindikiza katika sala zao katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.