2016-02-19 07:36:00

Papa Francisko "achonga" na waandishi wa habari!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 18 Februari 2016 amerejea kutoka Mexico alikokwenda kama mmissionari wa huruma ya Mungu na mjumbe wa amani. Baada ya kuwasili mjini Roma, alikwenda moja kwa moja kwenya Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma kwa ajili ya kumshukuru Mama wa Mungu na kuyakabishi matunda ya hija hii ya kitume nchini Mexico chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, afya ya Waroma.

Baba Mtakatifuakiwa njiani kurejea mjini Vatican amepata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari kwa takribani saa nzima na hivyo kumwezesha kujibu maswali kumi na mawili aliyoulizwa na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake. Mauaji ya kinyama yanayoendelea nchini Mexico; nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wa dogo; changamoto ya wahamiaji mintarafu kampeni za uchaguzi mkuu nchini Marekani.

Waandishi wa habari wameulizia pia kuhusu mkutano wa Baba Mtakatifu na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima; majadiliano ya Bunge la Italia kuhusu ndoa za watu wa jinsia moja; kanuni maadili katika kupambana na Virusi vya Zika vinavyotishia Injili ya uhai katika baadhi ya nchi; Mustakabali wa Bara la Ulaya; Yohane Paulo II na mahusiano yake na wanawake; hija za kitume za viongozi wa Kanisa zilizoratibiwa na Dr. Alberto Gasbarri na miwshoni, Ibada kwa Bikira Maria wa Guadalupe!

Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru na kumpongeza Papa Mstaafu Benedikto XVI aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho tanzu ya Kanisa aliyeshughulikia kashfa ya Maciel kwa ari na moyo mkuu na kabla ya kifo cha Yohane Paulo II wakati wa Njia ya Msalaba, akatamka wazi kwamba, kulikuwa kuna haja kwa Kanisa kusafishwa kutokana na uchafu uliokuwa umezagaa ndani mwake. Huu ukawa ni mwanzo kwa Kanisa kufungua malango ili kuangalia jinsi ambavyo kashfa ya nyanyaso za watoto wadogo zilizokuwa zinafanywa na Wakleri zilivyolichafua Kanisa.

Dhamana hii inaendelezwa kwa sasa na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amemteua Katibu mkuu mwambata wa Baraza la Kipapa la Mafundisho tanzu atakayeshughulikia kesi za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa kuwajalia viongozi ujasiri wa kuiona kashfa hii na kuanza kuifanyia kazi, kwani inasikitisha kuona kwamba, wakleri ambao wamepewa dhamana ya kuwaongoza watoto kwenda kwa Mungu wanageuka kuwa ni mashetani na wanyanyasi wa watoto hawa.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, ujenzi wa kuta za utengano umepitwa na wakati na badala yake, watu waanze mchakato wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu. Uhamiaji ni kati ya changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa, changamoto ambayo imevaliwa njuga na Bwana Donald Trump, moja ya wagombea uchaguzi mkuu nchini Marekani anayetaka kuwadhibiti wahamiaji mara tu atakapoingia Ikulu ya Marekani pamoja na kumshutumu Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni mwanasiasa jambo ambalo Baba Mtakatifu anasema ni asili ya binadamu kadiri ya mwana falsafa Aristotle. Wakristo wanachangamotishwa kujenga madaraja ya watu kukutana na wala si kuta za kuwatenganisha watu.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, mazungumzo kati yake na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima yamewajalia furaha ya ndani na kwamba, anatarajia kushiriki kikamilifu wakati wa maadhimisho ya Sinodi Mtambuka ya Kanisa la Kiorthodox kwa njia ya ujumbe na sala, ili Kanisa hili liweze kusonga mbele. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Tamko la kichungaji lililotolewa na viongozi hawa wawili halina mahusiano yoyote yanayounga mkono sera za kisiasa za Russia.

Baba Mtakatifu anasikitika kuona jinsi ambavyo baadhi ya viongozi wa Kanisa la Wagriki Wakatoliki wanvyodai kwamba wamesalitiwa na kudanganywa kutokana na Tamko la viongozi hawa lililotiwa mkwaju, mjini Havana, Cuba, hapo tarehe 12 Februari 2016. Tafsiri ya Tamko hili iliyotolewa na Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk ina mwelekeo potofu kidogo kwani anadai kuwa na umoja kamili na Khalifa wa Mtakatifu Petro, lakini wakati huo huo akitoa maoni yake binafsi, jambo ambalo ni haki kabisa. Tamko hili linaweza kuendelea kujadiliwa na kupembuliwa, lakini jambo la msingi ni watu kukumbuka vita na mateso ya wananchi wa Ukraine ambao hadi sasa imekuwa ni vigumu kutekeleza Mkataba wa Minsk ili amani iweze kupatikana.

Kuhusu mjadala wa ndoa za watu wa jinsia moja unaoendelea kwenye Bunge la Italia, Baba Mtakatifu anakaza kusema, Khalifa wa Mtakatifu Petro hana sababu ya kuingilia masuala ya kisiasa ya nchi yoyote ile, anafiriki na kutenda kadiri ya Mafundisho ya Kanisa. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafafanua kwamba, Mbunge Mkatoliki anapaswa kutenda kadiri ya dhamiri yake nyofu; dhamiri ambayo inapaswa kufundwa barabara ili iweze kuona jema la kukumbatia na baya la kuepuka.

Baba Mtakatifu anasema, utoaji mimba ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na kamwe haiwezi kuwa ni sababu msingi katika mapambano dhidi ya Virusi vya Zika. Hapa kuna haja ya kuwa makini na kanuni maadili. Wanawake wanaweza kukwepa kubeba mimba ili wasiwaambukize watoto wao Virusi vya Zika, lakini haikubaliki kimaadili kwa wanawake kutoa mimba ili kupambana na Virusi vya Zika. Utoaji mimba si tataizo la kitaalimungu bali ni tatizo la kibinadamu na kitabibu. Watu wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Kuhusu Tuzo ya Carlo Magno anayotarajiwa kukabidhiwa hivi karibuni anasema, itakuwa ni fursa ya kupyaisha tena Umoja wa Ulaya, ili kuimarisha na kukuza utamaduni na historia yake, ili kusonga mbele zaidi. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Waraka wa Kitume baada ya maadhimisho ya Sinodi mbili za Maaskofu kuhusu familia unatarajiwa kutolewa hivi karibuni pengine hata kabla ya maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, maandalizi ya wanandoa watarajiwa, malezi na makuzi ya watoto wao kiroho na kimwili; waathirika wa matatizo na changamoto za kifamilia; ukosefu wa fursa za ajira ni kati ya mambo msingi yatakayojadiliwa na Waraka huu wa kitume. Wanandoa walioachika wakaamua kuoa au kuolewa tena wanapaswa kusaidiwa ili waweze kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, lakini hii haimaanishi kwamba, wataruhusiwa kushiriki Komunio Takatifu, kwani hili nalo lingekuwa ni janga jingine katika maisha ya ndoa na familia.

Baba Mtakatifu Francisko anasema hakuna dhambi ya kuwa na urafiki na mwanamke na kwamba, anafahamu fika kuwa Yohane Paulo II alikuwa na urafiki na Anna Tymienicka, mwanafalsafa kutoka Marekani. Urafiki kati ya mwanaume na mwanamke unasaidia kukamilishana. Kuzini na mwanamke wa mtu ni dhambi. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, hata yeye ana urafiki mzuri na wanawake kama ilivyokuwa hata kwa watakatifu wengi ndani ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, ni hamu ya moyo wake kutembelea China, kukutana na kuzungumza na Imam wa Alzhar kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini yanayotekelezwa na Baraza la Kipapa  la Majadiliano ya kidini chini ya uongozi wa Kardinali Jean Louis Tauran. Baba Mtakatifu anasema, akiwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Guadalupe, amesali, ametafakari, ili kuombea amani, ustawi wa maisha na utume wa Kanisa; amewaombea wakleri na watawa ili waweze kuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa kadiri ya matakwa ya Kristo Yesu, mengine ni siri yake na Bikira Maria wa Guadalupe!

Mwishoni, Dr. Alberto Gasbarri amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko pamoja na watangulizi wake kama vile: Yohane Paulo II na Papa mstaafu Benedikto XVI waliomwamini na kumkabidhi dhamana ya kuratibu na kusimamia hija zao za kitume. Kwa muda wa miaka 27 amefanya kazi na Mtakatifu Yohane Paulo II, akiwa kijana mbichi kabisa. Anamshukuru na kumwombea Kardinali Tucci aliyemfundisha kazi hata akaweza kuitumikia Vatican kwa kipindi cha miaka 47 ya maisha yake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.