2016-02-19 15:09:00

Lindeni utu na heshima ya wananchi wa Mexico!


Baba Mtakatifu Frsancisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Mexico alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Wayesuiti wanaoishi na kufanya utume wao nchini Mexico, kwenye Ubalozi wa Vatican nchini humo. Baba Mtakatifu anawasihi Wayesuiti nchini Mexico kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kulinda, kuendeleza na kudumisha utu na heshima ya wananchi wa Mexico, hususan wale wanaoteseka. Baba Mtakatifu anawakumbusha kwamba, vijana nchini Mexico ni utajiri na rasilimali ya pekee, inayopaswa kuendelezwa: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu anawakumbusha kwamba, kwa kufanya hivi, wanadumisha utu wa Kristo unaojionesha kwa kila mtu nchini Mexico. Hii ni nchi ambayo inaonesha sura ya ujana inayopaswa kufanyiwa kazi kwa kudumisha utu na heshima yao, ili kamwe vijana hawa wasiishie kwenye mateso Msalabani na kuwaacha watesi wao wakiendelea kutumbua nchi!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, watu wanateseka Mexico, lakini kuna mambo mazuri na utajiri mkubwa na historia ya pekee, Amerika ya Kusini. Hii ni nguvu na jeuri ya wananchi wa Mexico. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wote hawa uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na waendelee kushughulikia mchakato wa kumtangaza Mwenyeheri Miguel Augustin Pro, kutoka Guadalupe, ili kadiri ya mapenzi ya Mungu, siku moja aweze kutangaza kuwa ni Mtakatifu. Katika mazungumzo haya, Wayesuit wanaoishi na kufanya kazi zao nchini Mexico walimpatia masalia ya Mwenyeheri Miguel aliyeuwawa kikatili kunako mwaka 1927, wakati wa madhulumu dhidi ya Wakatoliki yaliyoendeshwa na Plutarco Elìas Calles.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.