2016-02-19 15:22:00

Laudato si ni muhtasari wa Mafundisho Jamii ya Kanisa!


Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si ni muhatasari wa Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusu kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amedhaminisha kuitunza na kuiendeleza na kwamba, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kusimama kidete kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote. Kanisa katika yote haya linakazia kuhusu utu na heshima ya binadamu, mafao ya wengi yanayoongozwa na kanuni maadili; mshikamano unaojengeka katika kanuni auni; haki na amani; mambo ambayo yanaweza kuchunguzwa kwa kuangalia changamoto za Makanisa mahalia!

Kwa ufupi haya ndiyo mambo msingi yaliyochambuliwa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani wakati alipokuwa anashiriki kwenye kongamano lililokuwa linajadili kuhusu Wakatoliki, Ubepari na Mabadiliko ya tabianchi; kongamano ambalo limefanyika hivi karibuni huko New York, Marekani kwa kuwashirikisha wanafunzi kutoka Chuo kikuu cha Molloy, Rockville, Long Island, kichoko mjini New York, Marekani.

Kongamano hili limeratibiwa na Padre James Martin, SJ pamoja na wawezeshaji wengine wawili waliopembua kwa kina na mapana kuhusu Ukatoliki, Ubepari na Mabadiliko ya tabianchi. Utu wa binadamu una thamani kubwa inayopaswa kulindwa na kuheshimiwa na kamwe si jambo la kuchezewa! Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanakumbushwa kwamba, wanashiriki katika kazi ya uumbaji na umwilisho, changamoto kwa binadamu kuwa ni watunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote.

Kardinali Turkson anakaza kusema, kuna haja ya kuwa na uwiano mzuri kati ya maendeleo ya sayansi na teknolojia sanjari na ukuaji wa uchumi kwa kuzingatia pia tunu msingi za maisha ya kiroho. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanajikita kwa namna ya pekee katika utu, mshikamano, kanuni auni, haki, amani na utunzaji bora wa rasilimali ya dunia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu wote. Mshikamano ni kanuni inayowataka waamini kuonesha hali ya kujali wengine kwa mahitaji ya kizazi cha sasa na kile kijacho, hususan kwa kuwafikiria maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Waamini wasimame kidete kulinda na kutunza mazingira kwa kupunguza hewa ya ukaa ambayo kwa sasa imekuwa ni chanzo kikuu cha majanga na maafa yanayoendelea kuwatumbukiza watu katika umaskini wa hali na kipato. Utunzaji wa misitu sehemu mbali mbali za dunia, ni changamoto inayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee kwa kuzuia kuenea kwa jangwa duniani. Ongezeko la joto duniani ni hatari anasema Kardinali Turkson kwani kutapelekea kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari na matokeo yake ni maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake juu ya utunzaji wa Mazingira nyumba ya wote, Laudato si, anakazia umuhimu wa kuzingatia uchumi unaojali, unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa mahitaji msingi ya binadamu na kwamba, wafanyabiashara wazingatie mafao ya wengi wanapotekeleza dhamana na wajibu wao ndani ya jamii. Binadamu licha ya kuchangia katika uharibifu wa mazingira nyumba ya wote, lakini wana uwezo pia wa kulinda na kutunza mazingira, kwa kuchagua kilicho chema, kizuri na kitakatifu, tayari kurithisha vijana wa kizazi kipya mazingira bora zaidi kuliko yalivyo kwa nyakati hizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.