2016-02-18 15:03:00

Majadiliano na utamaduni wa watu kukutana ni muhimu kwa mafao ya wengi


Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Mexico, Jumatano tarehe 17 Februari 2016 amekutana na kuzungumza na ulimwengu wa wafanyakazi kwa kukazia majadiliano na utamaduni wa watu kukutana; kazi, makazi na ardhi; mambo makuu yanayowawezesha watu kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa familia na jamii inayowazunguka. Majadiliano ni muhimu sana ili kusonga mbele katika mchakato wa maboresho ya maisha pamoja na kuondokana na mipasuko ya kijamii; tayari kushikamana kwa pamoja ili kujenga leo na kesho iliyo bora zaidi.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mshikamano na mafungamano ya kijamii yanajikita katika mchakato wa mawasiliano; kwa kuheshimiana na kuthaminiana; mambo ambayo yanaweza kuboresha maisha ya watu wengi nchini Mexico. Vyama vya wafanyakazi si wapinzani wa Serikali, bali kwa pamoja wanapania kutafuta fursa na nafasi bora za kazi na kwamba, vyama hivi ni muhimu kwa vijana wa kizazi kipya, ambao wanahitaji elimu na majiundo makini yatakayowapatia stadi za maisha, tayari kujipanga kwa ajili ya maendeleo yao kwa siku za usoni.

Bila kuzingatia mambo haya makuu, vijana wengi watajikuta wakitumbukia katika umaskini, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na uhalifu. Ili kuwajengea wananchi wa Mexico, leo na kesho iliyo bora zaidi, Baba Mtakatifu anasema kuna haja ya kujikita katika majadiliano; upembuzi yakinifu sanjari na kutengeneza nafasi za ajira kwa vijana. Kwa bahati mbaya, dhana inayotawala kwa nyakati hizi ni umuhimu wa mtu, faida kubwa na dhana ya kubana matumizi; mambo ambayo yana athari kubwa katika kanuni maadili ndani ya makampuni. Lakini, ikumbukwe kwamba, uwekezaji makini ni ule unaofanywa kwenye rasilimali watu; kwa kutengeneza fursa za kazi na kuwaheshimu na kuwathamini wafanyakazi. Rasilimali fedha kisiwe ni kipimo pekee katika mchakato wa uzalishaji na huduma.

Baba Mtakatifu anasema, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanatoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili. Kanisa ni sauti ya Kinabii inayotaka kuwatetea wanyonge kwa kudumisha haki zao msingi na ni kwa ajili ya mafao ya wengi. Kazi inapaswa kujikita katika utu, ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa jamii bora zaidi; kwa kushikamana na kusaidiana, badala ya kumezwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu; utamaduni ambao ni matokeo ya mipasuko na kinzani za kijamii; hali inayotaka kuunda mafungamano mapya ya kitaifa.

Baba Mtakatifu anawauliza wafanyakazi nchini Mexico, Je, ni urithi gani wanaotaka kuwaachia watoto wao kwa siku za usoni? Unyonyaji, mishahara kiduchu; nyanyaso kazini, biashara haramu ya binadamu au watumwa wa kazi? Mambo msingi ambayo wafanyakazi wa Mexico wanapaswa kuacha kama urithi kwa watoto wao ni: kazi, nyumba na ardhi; kwa kujikita katika mchakato wa kulinda na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote, amani na utulivu kwani wao wanashirikishwa kikamilifu katika kazi ya Mungu. Kamwe wananchi wa Mexico wasithubutu kuwaachia wala rushwa na mafisadi nchi yao, wala kwa kuwa na ukosefu wa usawa kazini; watu wawe na ujasiri wa kutafuta mafao ya wengi, hata kama ikiwa itawabidi kujisadaka wenyewe.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mashindano yasiharibu mustakabali wa maisha ya wananchi wa Mexico. Rasilimali mtaji ni muhimu kwa ajili ya mafao ya wengi na wala si mbadala wa maisha na utu wa binadamu. Mtaji utumike kwa ajili ya huduma, tayari kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata fursa za ajira na vijana wanaendelea kuwa na ndoto ya leo na kesho iliyo bora zaidi; tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi yao. Wazazi na walezi wapate nafasi ya kukaa na watoto wao kwenye familia; huku wakijenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Hii ndiyo Mexico ambayo watu wengi wanataka kuiona ikiendelezwa na kudumishwa; kwa kuthamini utu wa binadamu kwa ajili ya mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.