2016-02-18 15:16:00

Changamoto katika ulimwengu wa wafanyakazi!


Askofu Msaidizi Cavazos Arizpe, Mwenyekiti wa Tume ya wafanyakazi, Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na ulimwengu wa wafanyakazi nchini Mexico, Jumatano tarehe 17 Februari 2016, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko ambaye kweli amekuwa ni Mmissionari wa huruma ya Mungu na mjumbe wa amani, kauli mbiu ambayo inaongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Mexico. Kwa uwepo wake kati yao, Familia ya Mungu nchini Mexico imepata hamasa na ari kuu ya kusonga mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili.

Binadamu ameumbwa na anapendwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, ekolojia ya kibinadamu na kijamii katika mahusiano yake ya ndani yanawaelekeza watu katika ulimwengu wa kazi unaoshiriki katika kazi ya uumbaji na maendeleo ya mtu binafsi. Ulimwengu wa kazi unapaswa kujikita katika maisha ya kiroho na kimwili; kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi badala ya kuwageuza watu kuwa ni walaji wa kupindukia bila kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu kwa sasa na kwa siku zijazo. Ulimwengu wa wafanyakazi unakabiliwa na matatizo na changamoto nyingi zinazopaswa kufanyiwa kazi ili kukuza uchumi na kuwa na kazi bora zaidi, inayowapatia wafanyakazi mshahara wa haki, mambo yanayoimarisha mafungamano na mahusiano ya wafanyakazi na waajiri wao, tayari kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu, kwaniukosefu wa fursa za ajira ni mtikisiko mkuu wa kibinadamu na maisha ya kijamii.

Waajiri kwa upande wao, wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa ujumbe wa matumaini kwa ajili ya ulimwengu wa wafanyakazi unaokabilina naa changamoto nyingi kwa wakati huu kutokana na umaskini, ukosefu wa fursa za ajira na hifadhi za kijamii. Bado utu wa binadamu haujapewa kipaumbele cha pekee katika ulimwengu wa wafanyakazi hata kama inafahamika kwamba, kazi ni kichocheo makini cha maendeleo ya watu. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanaendelea kukazia umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu wa binadamu na mafao ya wengi sanjari na kupambana na umaskini; changamoto inayohitaji mshikamano, uwajibikaji sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. 

Waajiri wanapaswa kujenga utamaduni wa majadiliano na mshikamano na wafanyakazi wao, ili kujenga jamii inayosimikwa katika haki, usawa na udugu. Utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknolojia; ekolojia, uhamiaji na usalama ni changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo. Waajiri wanataka kumwendeleza mfanyakazi kwa kujikita katika maadili, uwekezaji na mikakati endelevu, kwa kuwa na fursa za ajira sanjari na kuendeleza majadiliano.

Wafanyakazi kwa upande wao, wanakiri kwamba, mshikamano wa kijamii umeuwezesha mji huu kuanza tena kucharuka katika maendeleo kutokana na mazingira magumu ya kazi; kinzani katika tunu msingi za maisha; uwepo mkubwa wa familia tenge pamoja na ukosefu wa tunu msingi za maisha ya kifamilia, ambazo zingewawezesha watu kujenga na kudumisha utu, heshima na upendo. Pamoja na changamoto zote hizi, wafanyakazi wengi wameweza kusimama kidete katika maisha yao ya imani na wanamwomba Baba Mtakatifu kuendelea kuwategemeza kwa sala na sadaka yake. Wanataka watoto wao wawe kweli ni wachamungu; watu wenye utu na heshima kwa wengine sanjari na kushirikiana na wadau mbali mbali ili kweli Mexico iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Wanataka amani, mishahara ya haki na nafasi ya kukaa na familia zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.