2016-02-17 14:25:00

Ugonjwa wa Zika isiwe ni sababu ya kukumbatia utamaduni wa kifo!


Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anasema, ugonjwa wa Zika kwa wakati huu ni tishio na changamoto kubwa kwa Serikali za Amerika ya Kusini na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake. Hapa kuna haja ya kushirikiana na kushikamana na Shirika la Afya Duniani pamoja na Shirikisho la Afya Amerika ya Kusini ili kupambana na virusi vya Zika, ili visiendelee kuenea katika nchi nyingine na hivyo kuhatarisha zaidi maisha ya watu, hasa maskini, watoto na wazee.

Jumuiya ya Kimataifa isaidie kutoa vifaa tiba, habari na dawa kwa ajili ya kupambana na Virusi vya  Zika, kwa kuwahusisha watu watu wengi zaidi na kamwe asiwepo anayeachwa nyuma katika mapambano haya. Wanawake wajawazito na watoto wao ni waathirika wa kwanza wa mashambulizi ya Virusi vya Zika, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kutetea maisha ya watu.

Hapa uchunguzi wa Virusi hivi unapaswa kuendelea kufanywa ili kuwa na uhakika wa njia za maambukizi ya Virusi hivi kitaalam sanjari na kuheshimu maisha ya binadamu ambayo ni matakatifu kwa kutoa huduma makini kwa wanawake wajawazito na watoto badala ya kukimbilia suluhu ambazo zinaweza kukumbatia utamaduni wa kifo! Ujumbe wa Vatican unasikitishwa sana ya ombi lililotolewa hivi karibuni na Jumuiya ya Kimataifa la kutaka wanawake walioambukizwa virusi vya Zika kutoa mimba na kwamba, hili si jibu makini kwa ajili ya kukabiliana na Virusi vya Zika. Watu wapewe habari sahihi ya jinsi ya kujikinga na kuzuia kuenea kwa Virusi vya Zika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.