2016-02-17 11:10:00

Mexico inapaswa kusimikwa katika haki, amani na upatanisho!


Askofu Salvador Rangel Mendoza wa Jimbo Katoliki la Chilpancingo-Chilapa, Mwenyekiti wa Tume ya Maaskofu wa Mexico kwa ajili ya Wakleri na Watawa, Jumanne, tarehe 16 Februari 2016 amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kufika na kuwa kati yao, ili kuweza kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hii ni heshima kubwa kwani kwa uwepo wake, wanaimarika katika imani na kuendelea kukua na kukomaa katika matumaini, ili wote waweze kushikamana katika upendo kama Kanisa, huku wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Maaskofu wanasema, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko miongoni mwao ni chachu ya kuendelea kusonga mbele katika njia ya Injili ya furaha, ili kwenda pembezoni mwa maisha ya watu wa nyakati hizi, ili kuwashirikisha huruma na upendo wa Mungu, daima wakijikita katika ushuhuda wa kinabii, ili kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Mexico ambayo inapaswa kusimikwa katika haki, upatanisho na amani. Maaskofu wa Mexico wanakaza kusema, kwa uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko kati yao, wanauona Uso wa huruma ya Mungu, mwaliko wa kumgudua Mungu Baba, mwingi wa huruma na mapendo, ili wao pia waweze kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu; tayari kujifunza kusamehe na kuwa karibu na wengine, ili kweli ushuhuda wa maisha yao, uweze kuwa na mvuto na mashiko kwa jirani zao.

Katika Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko amemkumbuka kwa namna ya pekee Askofu mkuu mstaafu Carlos Quintero Arce wa Jimbo kuu la Hermosillo, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia tarehe 16 Februari 2016 akiwa na umri wa miaka 96. Baba Mtakatifu ameialika Familia ya Mungu nchini Mexico kusali kwa ajili ya kumwombea Marehemu Askofu mkuu Arce, ili aweze kupata pumzoko la amani baada ya maisha na utume wake miongoni mwa watu wa Mungu nchini Mexico

Itakumbukwa kwamba, Marehemu Askofu mkuu Arce alizaliwa tarehe 13 Februari 1920. Tarehe 8 Aprili 1944 akapewa Daraja takatifu la Upadre, Jimbo Katoliki la Guadalajara, Mexico. Tarehe 20 Machi 1961 akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Ciudad Valles na hapo tarehe 14 Mei 1961 akawekwa wakfu kuwa Askofu. Kunako tarehe 3 Machi 1966 akateuliwa kuwa Askofu mwandamizi wa Jimbo Katoliki Hermosillo na tarehe 18 Agosti 1968 akasimikwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Hermosillo. Hayati Askofu Arce ni kati ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican aliyeshikiri kikamilifu katika maadhimisho haya ambayo yamekuwa kweli ni kipindi cha neema na baraka kutoka kwa Mungu kwa ajili ya Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.