2016-02-17 14:10:00

Elimu makini ni mbinu mkakati wa kupambana na misimamo mikali ya kidini


Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales hivi karibuni alisema mapambano dhidi ya misimamo mikali ya kidini na kiimani yanawezekana kwa njia ya mfumo thabiti wa elimu inayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Matumizi haramu ya mitandao ya kijamii, yamepelekea vijana wa kizazi kipya kujikuta wakiwa wapweke kama watoto yatima na matokeo yake wamekuwa ni wahanga wa vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Nichols alikuwa akizungumza na wakuu wa shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Uingereza. Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya vijana 700 kutoka Uingereza wamejiunga na vikosi vya kigaidi kuendeleza mapambano huko Syria na Iraq, jambo ambalo linatishia usalama na maisha ya watu wengi duniani!

Kardinali Nichols anakaza kusema, waathirika zaidi ni vijana wenye umri kati ya miaka 14 hadi 15, wanaotekwa mawazo na kuanza kufundishwa mbinu za kigaidi. Hawa ni watoto ambao bado wako shuleni. Lakini hili ni kundi ambalo linajikuta sehemu kubwa ya maisha yake kwa siku likiwa linaogelea katika matumizi ya mitandao ya kijamii na huko huko linakutana na wajanja wanaoliingiza katika mawazo na hatimaye, vitendo vya kigaidi. Mitandao ya kijamii imegeuka kuwa ni “vijiwe” kwa vijana wengi wa kizazi kipya.

Mitandao ya kijamii leo hii inataka kujibu maswali msingi katika maisha ya vijana: kujiunga na kuunganishwa na wengine; kuwa na mawasiliano ya haraka pamoja  na kupata habari kwa haraka bila ya kupoteza wakati; vijana wanataka kuwa na kiongozi na kuwa na mahali pa kukita maisha yao. Vijana wana kiu ya kutaka kushirikisha mawazo na maoni yao na hatimaye wanataka kujiburudisha. Haya ni mambo ambayo vijana wasiokuwa na msingi na msimamo makini wa maisha, wanatafuta kutoka kwenye mitandao ya kijamii, ili kupata utambulisho wao na dhamana ndani ya jamii.

Kwa bahati mbaya, vijana ndio walengwa wakuu wa vikundi vya kigaidi vinavyotumia kwa kiasi kikubwa mitandao ya kijamii. Makundi haya hutumia ujumbe wenye mvuto na mashiko kwa vijana kiasi kwamba, wanabaki wakiwa wamechanganyikiwa hata wasifahamu jambo la kutenda. Kutokana na bahari ya habari duniani, wachunguzi wa mambo wanasema, inatosha mwezi mmoja kubadili mawazo ya kijana na kumwingiza katika vitendo vya kigaidi.

Kardinali Nichols anawataka wadau mbali mbali wa elimu kuhakikisha kwamba wanakuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya tunu msingi za maisha; mintarafu mafundisho ya Kanisa Katoliki. Viongozi wa elimu wawe na mvuto kwa wote na wala si kwa kikundo cha watu wachache. Shule na taasisi za elimu ziwe ni mahali pa kuwafunda vijana tunu msingi za maisha ya kiroho, kimwili na kiutu, ili kuwawezesha vijana hawa kupata nafasi na utambulisho wao duniani kwa kujenga na kudumisha mahusiano mema na watu mbali mbali. Shule ziwasaidie vijana kuwa na dira na mwelekeo sahihi wa maisha kwa siku za usoni. Wadau mbali mbali wawasaidie vijana kujenga mahusiano mema na Kristo kwa njia ya sala, tafakari na Sakramenti za Kanisa. Wadau wa elimu wakifanikiwa kufikia lengo hili, watakuwa wamewasaidia vijana wengi kutomezwa na makundi ya kigaidi na ukosefu wa misingi ya haki na amani; mambo yanayohatarisha amani na mafungamano ya kijami.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.