2016-02-17 14:37:00

Boutros Boutros Ghali, Katibu mkuu mstaafu wa UN amefariki dunia


Baba Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya msiba wa Boutros Boutros-Ghali aliyefariki dunia tarehe 16 Februari 2016 akiwa na umri wa miaka 93. Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, anamkumbuka kwa kwa namna ya pekee Hayati Boutros Boutros Ghali kutokana na huduma yake kwa nchi na kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Baba Mtakatifu anapenda kumhakikishia Katibu mkuu uwepo wake wa sala, ili kuiombea roho ya marehemu Boutros Boutros Ghali pumziko la amani na raha ya milele. Anapenda kuwaimarisha wote walioguswa na msiba huu kwa njia ya sala zake. Hayati Boutros Boutros Ghali alikuwa Katibu mkuu wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kutoka Barani Afrika aliyefanya kazi zake katika mazingira magumu kutokana na uwepo wa vita baridi katika Jumuiya ya Kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.