2016-02-16 10:42:00

Mashuhuda wa Injili ya familia!


Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na familia ya Mungu nchini Mexico, huko Tuxtla Gutièrrezi wakati wa hija yake nchini Mexico, Jumatatu tarehe 15 Februari 2016 amesikiliza shuhuda za wanafamilia wanne; walivyosaidiwa na jirani zao kuona tena upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao, kiasi cha kujisikia furaha ikibubujika tena mioyoni mwao.

Kutokana na vikwazo walivyonavyo katika maisha ya kiroho, hawawezi kushiriki kupokea Ekaristi Takatifu, lakini maisha na majitoleo yao kwa maskini, wagonjwa na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii yanawasaidia kujisikia kuwa kweli ni sehemu ya Fumbo la mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Wamejitahidi kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili na kweli wanamshukuru Mungu kwa kuwawezesha kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu ambaye anaendelea kutembea pamoja nao. Inapendeza kuwa na maisha ya ndoa na familia; Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo Mungu na jirani wanapewa kipaumbele cha kwanza!

Familia hizi zimeshuhudia jinsi ambavyo: umaskini, uhalifu pamoja na kutelekezwa na wazazi wao, kumewafanya wajisikie kuwa wapweke na wanyonge na matokeo yake wakajikuta wamemezwa na malimwengu na kuwa ni watumwa wa miili yao. Wakaona aibu ya kuzomewa na kukataliwa na jamii, kiasi cha kujikuta wanakumbatia utamaduni wa kifo kwa kutoa mimba mara kadhaa! Watu hawa wameonja tena huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa njia ya Kanisa. Leo hii ni watu wapya kabisa, wanaoendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Mashuhuda hawa wamesaidiwa kwa katekesi makini na endelevu, wakagundua ndani mwao chemchemi ya: Sala, Sakramenti za Kanisa na maisha ya kijumuiya. Kwa kupokea Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho, wameonja huruma ya Mungu na leo hii wanapenda kushuhudia kwa midomo na maisha yao! Mashuhuda hawa wanamwomba Baba Mtakatifu kuendelea kusali kwa ajili ya kuwaombea wanawake wengi wanaotumbukizwa katika utamaduni wa kifo, ili kweli waweze kutubu na kumwongokea Mungu tayari kuwa ni mashuhuda wa Injili ya uhai!

Baadhi ya wanafamilia wameshuhudia jinsi ambavyo wameonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao hata katika ulemavu walionao. Imani na matumaini yamewawezesha kujenga na kudumisha tunu bora za maisha, kiasi kwamba, hata katika ulemavu wao, wamekuwa ni Wainjilishaji wakuu miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Wanamwomba Baba Mtakatifu Francisko aendelee kuwakumbuka na kuwaombea vijana wanaojikuta wakimezwa na malimwengu ili waweze kugundua uso wa huruma ya Mungu, tayari kutubu na kumwongokea Mungu.

Familia imara na thabiti zinazojikita katika Sala, Sakramenti, Neno la Mungu na ushuhuda wa Injili ya Familia, zimeshuhudia jinsi ambavyo, kwa kipindi cha miaka hamsini wameweza kutembea kwa pamoja kama bwana na bibi, huku wakizungukwa na watoto ambao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wanamshukuru Mungu kwa zawadi ya imani na wazazi wao ambao kweli wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa, kiasi kwamba, wakajenga ndani mwao utamaduni wa sala, tafakari na maisha ya Sakramenti, chachu ambayo imewawezesha kushikamana katika raha na furaha, machungu na fadhahaa ya maisha katika kipindi cha miaka hamsini ya maisha ya ndoa na familia!

Wamekutana na kuonja ukarimu, upendo na huruma ya viongozi wa Kanisa, waliowaimarisha na leo hii ni mashuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu. Wanamwomba Baba Mtakatifu Francisko kuendelea kusali kwa ajili ya familia zinazoogelea katika shida na magumu ya maisha; katika umaskini na magonjwa pamoja na kukosa fursa za ajira. Watu wengi nchini Mexico wanateseka sana lakini hawa ni watu wenye imani na matumaini; wanaoendelea kurithisha tunu msingi za maisha ya kifamilia kwa vijana wa kizazi kipya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.