2016-02-16 14:43:00

Mapambazuko mapya ya majadiliano ya kiekumene!


Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Balozi wa Vatican nchini Russia anasema, mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima yamefanyika kati ya ndugu wawili katika imani kwa kukazia umuhimu wa waamini wa Makanisa haya kutembea kwa pamoja kama kielelezo cha majadiliano ya kiekumene sanjari na kushirikiana kikamilifu katika kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza sehemu mbali mbali za dunia.

Askofu mkuu Ivan Jurkovic anasema baadhi ya changamoto hizi ni kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; mauaji, madhulumu na nyanyaso dhidi ya Wakristo; vitendo vya kigaidi pamoja na umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Mazungumzo haya ni ushuhuda wa mabadiliko makubwa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, yaliyopelekea viongozi hawa wawili kuweka mkwaju katika Tamko la Kichungaji kwa ajili ya Makanisa haya mawili, tayari kushirikiana na kushikamana.

Huu ndio Uekumene wa damu unaoshuhudiwa na Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo wanaoendelea kumimina maisha yao kutokana na ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; damu yao ni mbegu ya Ukristo sehemu mbali mbali za dunia. Viongozi wa Makanisa haya wanaonesha umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana na kushirikiana ili kutafuta suluhu ya changamoto na matatizo yanayomkabili mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Tamko la kichungaji lililotolewa na viongozi hawa wa Makanisa ni alama ya mshikamano unaojali na kuguswa na matatizo pamoja na mahangaiko ya binadamu katika ulimwengu mamboleo. Ni kielelezo cha ukomavu wa imani na shughuli za kichungaji unaohitaji majibu ya pamoja hususan kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya Mpango wa Mungu kwa binadamu pamoja na umuhimu wa kuwa kweli ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili kwa watu wa nyakati hizi wanaoendelea kukengeuka na kutopea katika dhambi.

Askofu mkuu Ivan Jurkovic anakaza kusema, kuna haja kwa Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mbali mbali kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wakristo wanapaswa kushirikiana ili kushuhudia kwa pamoja Injili ya Kristo, kwa kutembea pamoja kama kielelezo cha mshikamano kwa kuvuka vikwazo vya mawasiliano, ili kweli cheche za mabadiliko ziweze kuanza kujionesha, kwa kutambua kwamba, wote ni Wakristo wanaotumwa kuinjilisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.