2016-02-16 10:21:00

Iweni mashuhuda wa Injili ya familia na huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 15 Februari 2016 amekutana na kuzungumza na umati wa familia huko kwenye Uwanja wa Victor Manuel Reyna, Tuxla Gutièrrez, wakati wa hija yake ya kitume nchini Mexico. Amewashukuru wanafamilia kwa uwepo, ushuhuda na ukarimu wao unaowawezesha wengi kupata chakula chao cha kila siku, hata kama bado wanakabiliwa na matatizo na changamoto nyingi katika maisha. Hiki ni chakula cha furaha, matumaini, ndoto na jasho kubwa kutokana na machungu, majaribu na hali ya kukata tamaa.

Baba Mtakatifu amewashukuru wanafamilia walioshirikisha ushuhuda wa furaha, fursa, matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha kwa kuonesha ujasiri unaobubujika katika majadiliano kati ya vijana wa kizazi kipya na wazazi wao, ujasiri ambao unamwilishwa katika mahusiano na mafungamano ya kijamii, tayari kujenga familia inayojikita katika tunu msingi za maisha ya Kikristo, kadiri ya ndoto ya Mungu kwa mwanadamu, licha ya dhambi na adhabu ya wazazi wa kwanza. Hapo kila kitu kilionekana kana kwamba, kimepotea na kuyeyuka kama ndoto ya mchana!

Nyakati zilipotimia, Mwenyezi Mungu alimtuma Mwanaye wa Pekee, Yesu Kristo, akaonesha ujasiri wa ajabu, ili kuwashirikisha upendo na majitoleo yake; akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kama chachu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu; kwa kufungua mbingu na dunia; nyoyo na mikono ya watu, tayari kuchuchumilia ujenzi wa misingi ya familia kwa kushirikishana na kushikamana; kwa kuganga na kuponya madonda ya moyoni sanjari na kuthubutu kusamehe saba mara sabini; ili kupyaisha maisha ya kifamilia!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, anaendelea kusali kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya wanaokosa ujasiri wa kufanya maamuzi magumu katika maisha, kwani mara nyingi wanajisikia kuwa wapweke, hawana watu wa kushirikishana nao matumaini, magumu na changamoto za maisha zinazowasibu bila kusahau hali ngumu ya maisha. Umaskini ni jambo ambalo linahatarisha si utu wa mtu bali hata maisha yake ya kiroho. Lakini, upweke ni hatari na kishawishi kikubwa katika maisha ya binadamu na matokeo yake ni kutumbukia katika majanga ya maisha yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu anasema hapa kuna haja ya kuwa na sheria na kanuni zinazomwezesha mwanadamu kupata mahitaji yake msingi; ili kila familia iweze kutoa fursa kwa watoto wao kupata elimu na kazi, ili kwa njia hii, familia ziweze kuwa ni chemchemi ya upendo wa Mungu unaomwilishwa katika huduma kwa jirani. Sheria na sadaka binafsi ni tunu msingi katika kupambana na majanga na maafa ya maisha. Waamini wanapaswa kusimama kidete kujenga, kudumisha na kushuhudia Injili ya familia; ili kweli familia ziweze kuchangia katika ustawi na maendeleo ya binadamu wote; badala ya familia kutengwa na kusukumizwa pembezoni mwa maisha ya kijamii!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kweli yataka moyo kuishi katika familia; kuna nyakati za raha na karaha; nyakati za furaha na machungu; lakini jambo la msingi kwa wanafamilia ni kuhakikisha kwamba, wanaendelea kushikamana katika upendo, msamaha na huruma; mambo msingi yanayodumisha na kujenga familia imara badala ya kujikita katika mambo ya nje! Baba Mtakatifu anaikumbusha familia ya Mungu nchini Mexico kwamba, inayo Mama Bikira Maria wa Gudalupe, anayewaombea na kuwategemeza wakati wa majanga ya maisha; wanapokuwa pweke na kwamba, yuko tayari kulinda na kuzitegemeza familia zao. Jambo la msingi ni wao kuwa na ujasiri wa kumpokea Kristo, Mtoto mpendwa wa Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.