2016-02-15 10:07:00

Papa Francisko kielelezo cha faraja na matumaini kwa wagonjwa!


Hospitali ya Watoto ya “Federico  Gomez”  iliyoko nchini Mexico baada ya kufanyiwa mageuzi na ukarabati mkubwa, kunako mwaka 1943 ikazinduliwa na kuwa ni kati ya Hospitali kubwa maalum kwa ajili ya huduma kwa watoto wanaosumbuliwa na ugonjwa wa Saratani na Dr. Federico Gomez akawa ni Mkurugenzi wake wa kwanza  hadi kufikia mwaka 1963. Hospitali hii ikawa ni kituo muhimu sana cha majiundo makini kwa madaktari wa watoto.

Hospitali hii ambayo imepewa jina la Federico Gomez ni kutambua mchango wa Dr. Gomes katika kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai kwa watoto wanaoteseka kwa ugonjwa wa Saratani. Hospitali hii ina vitanda 212 na kunako mwaka 1979, Mtakatifu Yohane Paulo II akaitembelea wakati wa hija yake nchini Mexico. Hospitali hii kwa mwaka inawahudumia watoto zaidi ya laki mbili na hamsini na tano elfu wanaopata huduma ya nje. Watoto wanaohudumiwa hapo hospitalini kwa kulazwa ni elfu sita kwa mwaka.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 14 Februari 2016 ametembelea Hospitalini hapo na kuzungumza na watoto wagonjwa kama afanyavyo Babu kwa wajukuu wake ili kuwaonesha watoto hawa matumaini na huruma ya Mama Kanisa katika shida na mahangaiko yao pamoja na kuwatia shime wazazi na walezi wa watoto hawa! Baba Mtakatifu anasema, lengo la kuwatembelea Hospitalini hapo ni kutaka kushirikishana maisha na watoto wagonjwa pamoja na wahudumu wao. Baba Mtakatifu anasema, hata Yesu alipokuwa Mtoto mdogo alitolewa na wazazi wake Hekaluni. Mzee Simeone akampokea, akashukuru na kumbariki Mtoto Yesu.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, yuko kati yao kama Mzee Simeone, ili kuwaangalia na kumshukuru Mungu kwa huduma makini inayoendelea kutolewa na wafanyakazi wa sekta ya afya Hospitalini hapo, ili kweli watoto hawa waweze kujisikia kwamba, wanahudumiwa vyema. Anapenda kuwapatia baraka ya Mungu wazazi na walezi wa watoto hawa wanaowashirikisha upendo na furaha ya ndani; huku wakiendelea kupata faraja na tunza ya Bikira Maria wa Guadalupe. Baba Mtakatifu anawaalika watoto, wazazi na wafanyakazi wa Hospitali hii, kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.