2016-02-15 09:33:00

Ni muda uliokubalika wa kuondokana na uchu wa mali, kiburi na umaarufu!


Kwaresima ni kipindi mahususi kinachowaandaa waamini kuadhimisha Fumbo la Pasaka, kilele cha huruma ya Mungu kwa binadamu. Ni wakati wa kukumbuka zawadi ya Ubatizo, pale waamini walipozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu na hivyo kufanyika kuwa ni wana wateule wa Mungu. Mama Kanisa anawaalika watoto wake kufurahia zawadi hii ya  imani kwa matumaini, kwa kutambua kwamba, wanapendwa na Mwenyezi Mungu anayetaka kuwavika vazi jipya linaambata utu na upendo mkuu.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kituo cha elimu ya juu huko Ecatepec, Mexico, Jumapili, tarehe 14 Februari 2016. Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, Mungu ni Baba wa wote anayetambua familia kubwa inayojikita katika udugu kwa kugawana na kushirikishana Mkate uliomegwa na kutolewa kwa ajili ya wengi.

Kila adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, ni kumbu kumbu endelevu kwa waamini kwamba, wao ni watoto wa Mungu, ushuhuda uliotolewa na Mababa wa imani, waliodiriki hata kuyamimina na wanaoendelea kumwaga damu yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kifamilia, msingi thabiti wa jamii imara.

Hii kamwe isiwe ni jamii kwa ajili ya wateule wachache  wakati umati mkubwa wa watu unaogelea katika dharau na nyanyaso kwa utu wao kutotambuliwa na kuheshimiwa kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu anayasema haya kwa uchungu mkubwa kutoka moyoni mwake! Kwaresima ni kipindi cha kufungua macho ili kuona ukosefu wa haki unaoendelea kutenda katika jamii ya watu, kiasi cha kuharibu ndoto ya Mungu kwa binadamu. Ni muda uliokubaliwa wa kuondokana na vishawishi vya utajiri, umaarufu na kiburi. Hivi ni vishawishi ambavyo Yesu alikumbana navyo Jangwani kabla ya kuanza maisha yake ya hadhara.

Kishawishi cha kwanza ni kutaka kumiliki utajiri na rasilimali ya dunia kwa mafao binafsi badala ya kutumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, kwani hii ni zawadi ya Mungu kwa wote. Ni kishawishi cha kutaka kujitajirisha kwa mgongo wa maskini na kwamba, katika jamii ya wala rushwa na mafisadi, hiki ndicho chakula wanachopewa watoto katika familia!

Kishawishi cha pili ni umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko, unaowadharau na kuwabeza watu wengine na matokeo yake, watu wanatumbukia katika kiburi kwa kujisikia kuwa ni bora kuliko watu wengine na kusahau kwamba, wao si mali kitu! Hivi ni vishawishi ambavyo Mkristo anakumbana navyo katika safari ya maisha yake ya kila siku; mambo ambayo kimsingi yanaharibu ile furaha ya Injili kwa mwamini kujikuta anakita maisha yake katika dhambi!

Waamini wanapaswa kujiuliza maswali kadhaa ili kuangalia ni kwa kiasi gani wanatambua uwepo wa vishawishi hivi katima maisha yao;  ni kwa kiasi gani mfumo wa maisha yao unawatumbukiza katika umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko kiasi hata cha kutumbukia katika kiburi kinachoharibu chemchemi ya maisha? Je, kama Wakristo wamejitahidi kuwahudumia jirani zao kwa njia ya matendo ya huruma; kwa kulinda utu wao na kuwasaidia kuonja furaha na kuwa na matumaini?

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, wamemchagua Kristo ambaye ameonesha umahiri mkubwa kwa kupambana na shetani kwa majibu yaliyokuwa yanabubujika kutoka katika Neno la Mungu. Hakuna mjadala na shetani, kwani daima anashinda, lakini kwa njia ya Neno la Mungu, mwamini anaweza kumbwaga shetani, kwa kusikiliza Neno la Mungu na kuendelea kumfuasa Kristo kwa uaminifu. Ikumbukwe kwamba, jina la Mungu ni huruma inayopaswa kumwilishwa kwa jirani kwani jina lake ni utajiri, ni umaarufu na ni nguvu; changamoto kwa waamini kujiaminisha kwa Mungu. Waamini wajazwe na furaha kila wakati wanaposhiriki maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.