2016-02-15 14:07:00

Mwaka wa huruma ya Mungu Tanzania unajikita katika Unjilishaji wa kina!


Askofu Gervas J. Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Mpanda katika mahojiano maalum na Radio Vatican anapembua kwa kina na mapana maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko, kipindi maalum cha toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji! Anagusi kwa kifupi Mwaka wa Watawa Duniani na Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Askofu Nyaisonga anasema, Familia ya Mungu nchini Tanzania inaadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kutambua kwamba, kama binadamu na waamini wanayodhamana ya kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, ili kuchuchumilia utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili. Waamini wanaalikwa kuwa na jicho la huruma kwa jirani zao. Mambo yote mawili yanapaswa kutekelezwa kwa kukimbilia kwenye kiti cha huruma ya Mungu pamoja na kuwasaidia wenye shida na mahangaiko mbali mbali ya maisha.

Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, imekuwa ni fursa ya kutafakari kwa kina na mapana maisha, utume, fursa na changamoto wanazokabiliana nazo watawa; mwaliko kwa waamini kuambata heri za mbinguni kwa kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Waamini wameungana na Kanisa zima katika maadhimisho haya ambayo yamekuwa kweli ni chachu ya kuwafahamu watawa na utume wao katika maisha ya Kanisa mahalia. Askofu Nyaisonga anasema, Bara la Afrika lilipata upendeleo wa pekee, kwa Baba Mtakatifu Francisko kuzindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati. Hii ni dhamana na changamoto kwa Familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba, inajikita katika kutafuta, kudumisha na kukuza misingi ya haki, amani na upatanisho kama kielelezo makini cha mchakato unaopania kumwilisha huruma ya Mungu katika maisha ya watu.

Kwaresima ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu unaongozwa na kauli mbiu ”Nataka rehema na wala si sadaka”. Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina kwa kumwangalia Bikira Maria, kielelezo cha Kanisa linaloinjilisha kwa vile limekwishainjilishwa. Ni wakati wa kutafakari Agano kati ya Mungu na binadamu linalojikita katika historia ya huruma ya Mungu inayomwambata mwanadamu mdhambi. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, Kwaresima ya mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu wanajitahidi kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Askofu Nyaisonga anasema, huu ni mwelekeo wa jumla unaotolewa na Baba Mtakatifu wakati huu wa kipindi cha Kwaresima. Lakini, familia ya Mungu nchini Tanzania ina vipuembele vyake. Inapenda kuangalia kwa namna ya pekee huruma ya Mungu na ufunuo wake katika maisha ya mwanadamu; jinsi ambavyo Kanisa la Tanzania linapenda kumwilisha huruma hii katika uhalisia wa maisha na utume wake kwa njia ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kupokea Sakramenti za Kanisa na kumwilisha Imani katika matendo; kielelezo cha toba ya kweli na wongofu wa ndani. Bikira Maria ni kielelezo cha huruma ya Mungu.

Kwa upande wake, Padre Felix Mushobozi, C.PP.S. anasema maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni wakati muafaka wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, utu na heshima ya binadamu, kwa kutambua kwamba, waamini kimsingi wanapaswa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa kwa njia ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani imekuwa ni changamoto kwa Watawa kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya furaha na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya huduma makini kwa maskini, daima wakiwa tayari kusoma alama za nyakati, ili watu wengi zaidi waweze kuguswa na kusukumwa kutafuta Ufalme wa Mungu katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.