2016-02-15 12:18:00

Kwaresima ni kipindi cha neema na baraka!


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, Kipindi cha Kwaresima ni wakati uliokubaliwa na Mama Kanisa kwa ajili ya toba, kufunga, kusali na kufanya majitoleo yanayomwilisha imani katika matendo ya huruma kiroho na kimwili, changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Ni wakati wa kujikita katika kusoma, kutafakari na kumwilisha huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa, ili kweli waamini waweze kuwa ni sura halisi ya Baba mwenye huruma aliyefunuliwa na Kristo Yesu. Hiki ni kipindi cha neema na baraka, changamoto kwa waamini kuwa na mwelekeo mpya wa maisha ya kiroho na kamwe wasifanye mambo kwa mazoea!

Askofu mkuu Ruwaichi anakaza kusema, Kwaresima ni kipindi cha kuwakumbuka, kuwaombea na kushikamana na wakristo wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa ajili ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Ni muda wa kujinyima na kuwasaidia Wakristo hao, lakini kwa namna ya pekee Wakristo wanaoishi katika Nchi Takatifu. Itakumbukwa kwamba, sadaka inayotolewa na waamini Ijumaa kuu ni kwa ajili ya kuwategemeza Wakristo wanaoishi Nchi takatifu, kumbe hapa waamini na watu wenye mapenzi mema wanaalikwa kuchangia kwa hali na mali.

Hawa ni Wakristo waliobanwa, wakajaribiwa na kutikiswa katika imani yao. Waamini wawakumbuke kwa sala na majitoleo wakristo wote wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi sehemu mbali mbali za dunia, ili neema, huruma na upendo wa Mungu uweze kuwaimarisha katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, ili kamwe wasikate tamaa wala kusaliti imani yao. Hiki ni kipindi ambacho Kanisa pia lina Sali kwa ajili ya umoja wa Kanisa, iwe ni fursa kwa wakristo kufahamu mambo msingi ili kushughulikia umoja wa Kanisa kwa vigezo ambavyo vitawasaidia Wakristo kweli kujikita katika mambo msingi katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.