2016-02-15 09:51:00

Jengeni mshikamano wa dhati ili Mexico iwe kweli ni Nchi ya ahadi!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kituo cha elimu ya juu huko Ecatepec, Mexico, Jumapili tarehe 14 Februari 2016, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, amefanya rejea kwenye Somo la kwanza kutoka katika kitabu cha Kumbu kumbu la Torati, pale Musa anapowataka Waisraeli kukumbuka historia ya maisha yao; kwa kuangalia magumu waliyokumbana nayo na jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu aliwaonesha upendo, huruma na ukarimu wake usiokuwa na mipaka.

Hii ni siku ya kumshukuru Mungu kwa wema na upendo wake kwa binadamu, mwaliko wa kukumbuka tamaduni, mapokeo, mila na desturi njema, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja na waja wake na kwamba, kumbu kumbu hai ya uwepo endelevu wa Mungu kati ya waja wake inajikita katika maisha ya watu; tamaduni, mapokeo na imani thabiti bila kusahau mshikamano na huruma yake kwa binadamu kwa kuwapatia nguvu ya kuwa na matumaini ya mwanzo mpya.

Baba Mtakatifu amewakumbusha maneno ya Mwenyeheri Paulo VI aliyewataka Wakristo wa Mexico kushikamana na wale wote ambao wanateseka kwa kukosa mahitaji yao msingi; hawana fursa za ajira na vijana wanaendelea kukosa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Wakristo wawe daima mstari wa mbele kushiriki katika mchakato wa maboresho ya maisha ya watu, kwa kumwona na kumtambua Kristo anayejionesha kati ya watu wake.

Wakristo nchini Mexico wajifunge kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, Mexico inakuwa ni nchi ya ahadi, kwa watu wake kuendelea kubaki nchini mwao bila ya kulazimika kuhama wala kuikimbia nchi yao. Mahali ambapo kazi inakuwa ni utambulisho na utimilifu wa maisha ya binadamu na wala si chanzo cha unyonyaji; Mexico iwe ni nchi ambako watu wake wanajifunga kibwebwe kupambana na umaskini badala ya utajiri na rasilimali ya nchi kuwanufaisha watu wachache. Mexico iwe ni nchi ambayo hakuna sababu tena ya wazazi kulalama kutokana na watoto wao kutumbukizwa katika biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Baba Mtakatifu anasema, Mexico ina harufu ya Bikira Maria wa Guadalupe, kielelezo cha upendo, changamoto kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa umoja, huduma, imani thabiti; ukarimu, haki na upendo kwa maskini, ili kweli Injili ya furaha iweze kufika hadi miisho ya dunia na kamwe hasiwepo mtu anayekosa mwanga wa Injili ya Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.