2016-02-15 10:24:00

Askofu mkuu Ivan Jurkovic ateuliwa kuwa Mwakilishi wa kudumu UN, Geneva


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Ivan Jurkovic kuwa Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss. Hadi kuteuliwa kwake, Askofu mkuu Jurkociv alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Russia na Uzbekistan. Alizaliwa tarehe 10 Juni 1952 huko Slovenia. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi akapadrishwa tarehe 29 Juni 1977. Tarehe 28 Juni 2001 akateuliwa kuwa Askofu.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Jurkovic amekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene uliohitimishwa mjini Havana, Cuba kwa Baba Mtakatifu Francisko kukutana na kuzungumza na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima, viongozi wa Makanisa walioandika ukurasa wa historia mpya ya majadiliano ya kiekumene. Askofu mkuu Jurkovic anachukua nafasi ya Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi ambaye ameiwakilisha Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva tangu mwaka 2003. Katika utume wake wa Kidplomasia, Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi amewahi kuwa ni Balozi wa Vatican nchini Ethiopia na Eritrea.

Askofu mkuu Jurkovic anasema, mkutano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima ni tukio ambalo limekuwa na mvuto mkubwa si tu kwa Wakristo wa Makanisa haya mawili, bali chachu na changamoto ya viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa kujenga utamaduni wa kukutana na kuzungumza uso kwa uso ili kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa zilizopo katika maisha ya watu badala ya kuendelea kujenga kuta zinazowatenganisha watu!

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walianzisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene na Mwenyeheri Paulo VI akakutana na kuzungumza na Patriaki Athenagora, picha ambayo imejirudia tena huko Havana, Cuba, kwa Baba Mtakatifu Francisko kukutana na kuzungumza na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima. Hiki ni kielelezo cha ukomavu na ujasiri wa kiimani; tukio ambalo limekuwa ni faraja kubwa kwa Wakristo na wapenda amani sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni alama ya matumaini mapya katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kwa Makanisa kutembea na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Tamko la kichungaji ni dira na mwelekeo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa haya mawili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.