2016-02-14 11:03:00

Waonjesheni watu wa Mungu huruma na upendo!


Baba Francisko, Jumamosi, tarehe 13 Februari 2016 amekutana na Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Kupalizwa mbinguni. Amesali na kuzungumza na Maaskofu, huku akikazia kwa namna ya pekee umuhimu wa Ibada na Liturujia katika maisha ya Wakleri na kwamba, wananchi wa Mexico wana ibada ya pekee kabisa kwa Bikira Maria wa Guadalupe, hii ndiyo siri ya maisha yao ya kiroho, inayopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kutokana na utete wake katika maisha ya watu. Hapa kuna haja ya kutembea kwa uchaji na unyofu, ili kufungua lango la siri ya maisha ya watu inayofumbatwa katika sakafu ya mioyo yao, ili kuwafunulia watu sura ya fumbo hilo katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anawaambia Maaskofu kwamba, njia pekee ya kuweza kuwa na maridhiano ya kweli na waamini wao ni kuwaonesha upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao; huruma ambayo ina nguvu ya kuweza kufungua na kufunga nyoyo za watu na wala si ukali wa sheria, bali unyenyekevu unaoshuhudiwa katika huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anawaambia Maaskofu kamwe wasiogope kushuhudia ukweli na uwazi katika maisha na utume wao kwani Kanisa halina sababu ya kufanya kazi na kutekeleza utume wake katika kificho!.

Wakleri wasikubali hata kidogo kumezwa na malimwengu na vishawishi vinavyofanywa kwa njia ya mikataba ya kisirisiri na wala wasijiaminishe na kuweka matumaini yao kwenye “Farasi na Wapanda farasi”  wa Farao wa nyakati hizi kwani nguvu ya Wakleri anasema Baba Mtakatifu inajificha katika wingu la moto linalopasua bahari na kugawa maji sehemu mbili, bila kupiga makelele! Viongozi wa Kanisa wasikubali kupoteza nguvu kwa mambo yasiyokuwa na msingi, kwa mazungumzo yasiyokuwa na tija wala mashiko; kwa kujikita katika mipasuko na mitafaruku ya kijamii; kwa kuzama na kupotelea katika uchu wa mali na madaraka; kwa sera na mikakati inayoelea kwenye ombwe! Au kwa kujishikamanisha na makundi kwa ajili ya kulinda na kutetea mafao binafsi.

Baba Mtakatifu anawaalika kwa namna ya pekee Maaskofu kujifunza historia ya mambo yaliyopota, kwa kuangalia mchango wa Mababa wa imani kutoka Mexico, jinsi walivyojitahidi kuandaa vijana wa kizazi kipya kuweza kuzama katika fumbo la huruma ya Mungu; kwa kujifunza na hatimaye kuwafundisha wengine kanuni msingi katika kujadiliana na Mwenyezi Mungu. Maaskofu wawe na jicho la pekee kwa wenyeji wa Mexico; kwa kutambua utajiri unaofumbatwa katika maisha yao, tayari kushiriki katika utambulisho unaounda taifa moja tu na wala si vinginevyo!

Maaskofu kamwe wasichoke kuwakumbusha waamini wao umuhimu wa mizizi ya zamani katika maisha ya kiroho, iliyowawezesha kuwa na muhtasari wa maisha ya Kikristo yanayomwilishwa katika ubinadamu, utamaduni na maisha ya kiroho; mambo yanayoendelea kushamiri kwa namna ya pekee nchini Mexico. Maaskofu wawe na ujasiri wa kuangalia mbele kwa kujichotea utajiri katika mambo ya kale, ili kuboresha ya sasa na hatimaye, kuwa na mwanga angavu kwa siku za usoni. Maaskofu wawe makini katika mchakato wa kuimarisha imani, kwa kuthamini ibada za waamini wao; kwa kuondokana na ubaridi wa maisha ya kiroho; kwa wakleri kutaka kukumbatia yote; kwa tabia ya kutojali wala kuthamini watu; kwa kujitafuta na kutafuta sifa bandia.

Baba Mtakatifu anawataka Wakleri kuonesha upendeleo wa pekee kwa kila mwamini mmoja mmoja anayemtafuta Mungu katika maisha yake; wajitahidi kusoma alama za nyakati ili kutambua mahangaiko na mahitaji msingi ya binadamu. Waamini kutaka kukutana na Mungu ni hali ambayo iko moyoni mwa Mungu mwenyewe. Bikira Maria wa Guadalupe aliomba kujengewa “kibanda”, lugha inayoeleweka na kutumiwa sana na wananchi kutoka Amerika ya Kusini; hii ndiyo kiu yao, vinginevyo wanaogopa kupoteza mwelekeo wao wa maisha!

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anawaalika Maaskofu kuwa na dira na mwelekeo wa pamoja kwa kumwangalia Bikira Maria wa Guadalupe; ilikutekeleza utume na maisha ya Kanisa kadiri ya mwelekeo huu, kwa kushikamana katika umoja kati ya Maaskofu wenyewe; Maaskofu na Mapadre wao pamoja watu katika ujumla wao. Maaskofu wawe na sera na mikakati makini kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji pamoja na kuimarisha ushirikiano wa dhati na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, iko siku Mexico na Kanisa lake, itaweza kufika kwa wakati kwa ajili yake, historia na kwa Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.