2016-02-14 10:44:00

Pambaneni na rushwa, dawa za kulevya na ubaguzi wa watu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 13 Februari 2016 amewasili nchini Mexico na kukutana na bahari ya watu waliofika kumlaki kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa wa “Benito Juarez” ulioko Mexico City. Rais Enrique Penà Nieto wa Mexico ameongoza ujumbe wa viongozi wa Serikali na Kanisa na baadaye viongozi hawa wawili wakapata nafasi ya kuteta kwa faragha. Baba Mtakatifu baadaye amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, wanasiasa na wanadiplomasia wanaowakilisha mataifa yao nchini Mexico.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewaambia wenyeji wake kwamba, yuko nchini Mexico kama mmissionari wa huruma ya Mungu na mjumbe wa amani, kauli mbiu inayoongoza hija yake ya kitume nchini Mexico. Baba Mtakatifu anasema, yuko Mexico kwani anataka kwenda kutembelea na kusali kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Guadalupe, ili kumwangalia na hatimaye, kumwachia nafasi, Mama ili aweze kumwangalia mwanaye kwa jicho la huruma, upendo na tunza ya kimama. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, Mexico ni nchi ambayo imebahatika kuwa na fursa, utajiri na rasilimali nyingi pamoja na kwamba, Mexico ni njia panda ya Bara la Amerika. Mexico imebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa watu na tamaduni zao, rasilimali inayoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya wengi. Lakini, utajiri mkubwa Mexico kuliko kitu kingine chochote kile ni vijana wanaounda asilimia kubwa ya wananchi wote wa Mexico.

Kwa njia hii, Mexico inaweza kujiwekea mbinu mkakati wa maendeleo kwa sasa na kwa siku za usoni. Hii ni dhamana na changamoto kwa wananchi wote wa Mexico kuhakikisha kwamba wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa nchi yao kwa kuwekeza zaidi miongoni mwa vijana. Hapa Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee mafao ya wengi, ambayo kwa bahati mbaya katika karne ya ishirini na moja mafao ya wengi hayajapewa kipaumbele cha kutosha na matokeo yake ni upendeleo, mafao ya watu wachache ndani ya jamii na matokeo yake ni kujengeka kwa tabia ya rushwa, biashara haramu ya dawa za kulevya na ubaguzi wa watu na tamaduni zao.

Huu ni mwanzo wa machafuko ya kijamii, biashara haramu ya binadamu, utekaji nyara pamoja na kukumbatia utamaduni wa kifo unaosababisha mateso na mahangaiko ya wengi sanjari na kukwamisha mchakato wa ukuaji wa maendeleo ya watu. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, nchini Mexico, kuna mashuhuda wa kiraia ambao wamegundua kwamba ili kuondokana na hali ya maisha inayojikita katika ubinafsi, kulikuwa kuna umuhimu wa pekee wa kuanzisha makubaliano ya taasisi za kisiasa, kijamii na soko, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anasema, kwa kuzingatia rasilimali watu, kuna haja ya kuanzisha mchakato mpya wa majadiliano na makubaliano ili kujenga madaraja yatakayoimarisha mshikamano na wote ili kujenga jamii ambamo kila watu wanaheshimiwa na kuthaminiwa na wala hakuna mtu anayejisikia kuwa ni mhanga wa utamaduni wa ubaguzi na hali ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Viongozi wa serikali, wanasiasa, wasomi na viongozi wa kijamii wanapaswa kutekeleza dhamana na nyajibu zao kwa kushirikiana na kushikamana ili kutoa fursa kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika mustakabali wa nchi yao. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ili kufanikisha dhima hii, kuna haja ya kuwafunda watu kuwajibika barabara katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha hotuba yake kwa viongozi wa serikali, wanasiasa, wasomi na wanadiplomasia huko Mexico kwa ujumbe wa matumaini kwamba, anatembelea Mexico kama mmissionari wa huruma ya Mungu na hujaji anayepania kupyaisha pamoja nao mang’amuzi ya huruma ya Mungu, mwelekeo mpya unaowezekana kutekelezwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.