2016-02-14 11:19:00

Madhabahu ya Mungu ni maisha ya watu wake!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni tarehe 13 Februari 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria wa Gudalupe nchini Mexico; Ibada ambayo ilitanguliwa na maandamano makubwa, kielelezo kwamba, Bikira Maria ni alama ya kimama ya huruma na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amejikita zaidi katika tukio la Bikira Maria kumtembelea binadamu yake Elizabeth, kwa haraka ili kumsaidia kwani alikuwa ni mjamzito, kielelezo cha majitoleo na sadaka ya Bikira Maria kwa Mungu na kwa ndugu zake; Bikira Maria anayetaka kukutana na wengine! 

Kanisa kuu la Bikira Maria wa Guadalupe ni mahali ambapo Bikira Maria aliamua kuwatembelea wananchi wa Mexico kwa kumtokea Mtakatifu Juan Diego, akatumia lugha mahalia ili kuwahudumia wananchi wa Tepeyac. Uamuzi wa kumtumia Juan Diego ni uamuzi wa pekee unaoonesha kwamba, Bikira Maria ni kwa ajili ya watu wote wenye mapenzi mema na wala si kwa ajili ya kuwabeza baadhi ya watu!

Kwa tukio hili Juan Diego akawa kweli ni mjumbe wa imani na matumaini kwa wananchi wa Mexico, tangu Desemba 1531. Mwenyezi Mungu akaamsha na anaendelea kuamsha matumaini kwa maskini, wagonjwa, watu wasiokuwa na makazi bila kuwasahau wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kudhalilishwa na kukosa nafasi katika ulimwengu mamboleo. Ni matumaini kwa wazazi ambao wameshuhudia watoto wao wakitoweka bila kurejea tena nyumbani; wakitumbukizwa katika vitendo vya kihalifu. Hawa ni watu ambao wameonja matumaini na huruma ya Mungu katika maisha.

Juan Diego aliteuliwa na Bikira Maria ili kukesha, kutunza, kuhifadhi na hatimaye kujenga Madhabahu ya Bikira Maria wa Gudalupe. Hakua msomi wala hakuwa na nafasi ya pekee katika jamii, lakini huyu ndiye Bikira Maria aliyeamua kumchagua vinginevyo angemchagua mtu mwingine anasema Baba Mtakatifu, ili aweze kuwa ni mjumbe  wa Bikira Maria wa Gudalupe. Kwa njia yake, akathubutu kujenga upendo na haki unaojikita katika madhabahu ya maisha ya waamini katika jumuiya, jamii na tamaduni na kwamba, hakuna hata mtu mmoja ambaye amefungiwa nje!

Waamini wanakumbushwa kwamba, Madhabahu ya Mungu ni maisha ya watu wake; hususan vijana wasiokuwa na mwelekeo wala dira sahihi ya maisha; wazee waliotelekezwa na kusahaulika. Madhabahu ya Mungu ni familia zinazoteseka na kuhangaika; madhabahu ya Mungu ni watu mbali mbali ambao waamini wanakutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku! Lakini ikumbukwe kwamba, matumaini ni nguvu inayoweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu! Hapa jambo la msingi ni kuwa kimya na kumwangalia Bikira Maria bila kusema neno, kwa kumwomba ili aweze kuwapatia ulinzi na tunza ya kimama pasi na woga kama alivyofanya kwa Mtakatifu Juan Diego. Waamini wajifunze kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa jirani zao wanaokutana nao kila siku ya maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.