2016-02-13 14:46:00

Mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika maisha!


Padre Federico Lombardi Msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, mkutano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima umekuwa ni tukio la kihistoria  kama changamoto ya kutekeleza lile agizo la Kristo linalowataka wafuasi wake wawe wamoja kama Kristo alivyo na umoja na Baba yake wa mbinguni; Sala ya Kikuhani aliyoitoa Siku ile iliyotangulia kuteswa na kufa kwake Msalabani.

Imepita miaka mingi ambamo Wakatoliki na Waorthodox wamekuwa wakiishi katika mipasuko ya kiimani, kwa kutoelewana wala kushirikiana. Miaka elfu moja si haba anasema Padre Lombardi kwa viongozi wakuu wa Makanisa haya kuweza kukutana ana kwa ana, kuzungumza na hatimaye, kutoa Tamko la pamoja kuhusu shughuli za kichungaji. Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amebahatika kukutana na kuzungumza na Mapatriaki mbali mbali, lakini hii ni mara ya kwanza katika historia kwa Baba Mtakatifu kukutana na kuzungumza na Patriaki wa Moscow.

Mazungumzo haya yamefanyika tarehe 12 Februari 2016 mjini Havana, Cuba kwa kufungua ukurasa mpya wa majadiliano ya kiekumene, yenye mwelekeo mpana zaidi kwa kuonesha upya wa mchakato huu ambao umepata mwanzo wake nchini Cuba, ikilinganishwa na Bara la Ulaya ambalo kwa sasa linakabiliwa na changamoto kibao! Cuba imekuwa na upendeleo wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa tangu wakati wa Mtakatifu Yohane Paulo II, Papa mstaafu Benedikto XVI na kwa sasa katika kipindi kifupi, Baba Mtakatifu Francisko ametembelea Cuba mara mbili katika matukio ambayo kweli yanagusa akili na nyoyo za wengi. Baba Mtakatifu ameweza kukutana na kuzungumza na ndugu yake katika Kristo, Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima.

Padre Lombardi anaendelea kukaza kwa kusema kwamba, hizi ni juhudi za Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican waliotaka kuona Kanisa linavuka vikwazo kwa mipasuko na kinzani, tayari kuanza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili wote wawe wamoja tayari kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Hapa Kanisa linaendelea kutekeleza utashi wa Kristo, ili wote wawe wamoja, tayati kusimama kidete kupambana na changamoto za ulimwengu mamboleo kama vile: vita, magonjwa, umaskini, njaa, wahamiaji pamoja na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Hapa anayeshughulikiwa ni binadamu na utu wake; binadamu mzima: kiroho na kimwili.

Mazungumzo haya yenye mwelekeo wa kiekumene kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Kirill wa Moscow yamefanyika wakati ambapo Kanisa la Kiorthodox linajiandaa kuadhimisha Sinodi mtambuka; tukio ambalo pia limeshuhudia Makanisa haya yajikitahidi kutembea kwa pamoja kwa miaka mingi; kumbe, hata Kanisa Katoliki linaweza kuonesha uwepo wake wa karibu na endelevu katika matukio kama haya! Mkutano huu umekuwa ni tukio la furaha, imani na matumaini yanayozima kiu ya wengi waliokuwa wanasubiri nafasi kama hii. Tangu awali kumekuwepo na nia ya viongozi hawa wawili wa Kanisa kukutana na kuzungumza, Cuba imekuwa ni fursa kwa viongozi hawa kukutana kwa pamoja! Ni matumaini ya Padre Lombardi kwamba, hija hii ya kiekumene, itayawezesha Makanisa haya mawili kwenda mbali zaidi, ili siku moja yaweze kuwa ni umoja kamili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.