2016-02-13 10:10:00

Hili ni Tamko la Kichungaji!


Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kuelekea nchini Mexico, alipata tena fursa ya kukutana na kuzungumza na waandishi wa habari walioko kwenye msafara wake, ili kuonesha ile furaha iliyokuwa inabubujika moyoni mwake baada ya kukutana na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima; wakazungumza na hatimaye, kutia sahihi Tamko la pamoja katika maisha na utume wa Makanisa haya mawili sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu amewaambia waandishi wa habari kwamba, Tamko hili ni utajiri mkubwa ambao wataufanyia kazi kwa nyakati tofauti.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee kabisa, ameonesha moyo wa shukrani kwa Rais Raul Castro wa Cuba kwa ukarimu, mapokezi na dhamana aliyojitwalia, ili kuhakikisha kwamba, mazungumzo kati ya viongozi hawa wawili wa Makanisa yanafanikiwa kama ilivyojitokeza. Baba Mtakatifu anampongeza sana Rais Castro kwa kufanikisha tukio hili la kihistoria kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mazungumzo yake na Patriaki Kirill wa Moscow yamefanyika katika udugu; kwa kugusia mambo msingi yanayoyatatiza Makanisa haya mawili na kuzungumzia katika hali ya ukweli na uwazi. Wote wawili wamejisikia kuwa ni ndugu wa imani. Maaskofu wawili wanaojadiliana kuhusu maisha na utume wa Makanisa yao; viongozi wa kidini wanaopembua fursa, changamoto na matatizo yanayomkumba binadamu katika ulimwengu mamboleo. Vita inatotishia usalama na maisha ya wote; hali na maisha ya Kanisa la Kiorthodox, Sinodi mtambuka ya Kanisa la Kiorthodox.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, ndani mwake alijisikia kuwa na kisima cha furaha kilichokuwa kinabubujika kutoka kwa Kristo Yesu; wote wakazungumza katika misingi ya: uhuru, ukweli na uwazi. Wakalimani wamefanya kazi yao barabara; mazungumzo ambayo yameshuhudiwa na macho sita. Haya ni majadiliano yaliyowahusisha pia Askofu mkuu Hilarion na Kardinali Kurt Koch. Mazungumzo haya yamejikita katika uhuru kamili.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwa pamoja wamejiwekea mpango mkakati utakaotekelezwa na waamini wa Makanisa haya wakati wa hija yao ya majadiliano ya kiekumene, kwani umoja unajengwa kwa kutembea kwa pamoja. Wakati fulani majadiliano haya yalikuwa yanafanyika kwenye Maktaba, kwa kujikita katika masuala ya kitaalimungu; lakini katika mapambazuko mapya, majadiliano ya kiekumene yanafanyika kwa Wakristo kutembea kwa pamoja, ili hata Kristo atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu, awakute wakiwa wanatembea pamoja!

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Tamko la pamoja lililotolewa si tamko la kisiasa wala kijamii, bali ni Tamko la shughuli za kichungaji linalogusa mambo msingi katika maisha ya mwanadamu; utu na heshima yake; fursa, matatizo na changamoto katika maisha na utume wa Makanisa haya mawili. Baba Mtakatifu anakaza kusema, amebaki na furaha na amani kubwa moyoni mwake! Waandishi wa habari wanaweza kufanya kadiri wanavyoona inafaa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.