2016-02-13 14:57:00

Cuba ni daraja la watu kukutana!


Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kuelekea Mexico amemtumia  Rais Raul Castro wa Cuba, salam, shukrani na matashi mema; huku akiombea amani, ustawi na maendeleo kwa nchi ya Cuba na watu wake. Anasema, anakwenda Mexico kama mmissionari wa huruma na mjumbe wa amani. Kwa namna ya pekee, anapenda kumshukuru kwa ukarimu ambao Familia ya Mungu nchini Cuba imemwonesha alipotua kwa kitambo kifupi hapo Uwanja wa Ndege wa Havana.

Baba Mtakatifu anasema, safari hii imemkumbusha ukarimu na mapokezi makubwa aliyopata wakati alipotembelea Cuba kwa mara ya kwanza mwezi Septemba 2015. Anamshukuru Rais na Serikali yake kwa kuwezesha kufanikisha mkutano kati yake na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima. Huu umekuwa ni mkutano wa kihistoria na kwamba, kuna matumaini kuwa utaweza kuzaa mambo makubwa kwa siku za usoni. Majadiliano na ujenzi wa madaraja ya watu kukutana ni muhimu sana, ili kujenga na kuimarisha amani, upatanisho na maridhiano kati ya watu. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wananchi wote wa Cuba uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na kwamba, anawabeba moyoni mwake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.