2016-02-12 12:33:00

Safari njema huko Cuba na Mexico!


Baba Mtakatifu Francisko ameondoka mjini Roma kuelekea nchini Mexico kwa kutua kwanza kabisa nchini Cuba, ili kukutana na kuzungumza na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima, Ijumaa tarehe 12 Februari 2016. Kwenye Uwanja wa Ndege wa Fiumicino, viongozi mbali mbali wa Serikali ya Italia na Kanisa wamemsindikiza na kumwona Baba Mtakatifu akianza hija yake ya kumi na mbili kimataifa kuelekea nchini Mexico.

Rais Sergio Mattarella wa Italia amemwandikia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe wa shukrani na matashi mema nchini Mexico baada ya kufanya hija ya kitume mwezi Julai 2015 huko Equador, Bolivia na Paraguay; Cuba na Marekani mwezi Septemba 2015. Italia na Jumuiya ya Kimataifa anasema Rais Mattarella inaiangalia hija hii ya kitume kwa jicho la matumaini huko Amerika ya Kusini. Mexico ni nchi ambayo licha ya magumu na changamoto zake, ina utajiri mkubwa na rasilimali nyingi zinazoweza kutumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Hii ni hija ya matumaini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; ujumbe wa Baba Mtakatifu unaojikita katika: amani, mshikamano na matumaini ni muhimu sana katika maisha ya wananchi wa Mexico. Italia na Jumuiya ya Kimataifa ina matumaini makubwa kwa mkutano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima, ili kujenga na kudumisha majadiliano ya kiekumene pamoja na majadiliano kwa wale wote wanaoamini katika dhana hii. Rais Sergio Mattarella anamtakia Baba Mtakatifu safari njema na mafanikio mema katika safari yake ya kitume Cuba na Mexico katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.