2016-02-12 14:47:00

Papa safarini kuelekea Mexico


Baba Mtakatifu Francisko, Mapema ijumaa hii alianza safari kuelekea Mexico, kwa ajili ya Ziara yake ya Kimatiafa ya 12 ya Kitume ,  ambako atakuwa hadi Jumatano ijayo tarehe 18 Februari 2016. Kama kawaida akipita katika anga za nchi mbalimbali , kwa njia ya telegram alipeleka salaam zake za matashi mema kwa  wakuu wa nchi  na wanachi kwa ujumla.  Akiruka katika anga la Italia , alimsalimia Rais Sergio Mattarella, akisema ”ninapoondoka  Roma kuelekea  Mexico, kwenda kusaidia kanisa mahalia,  kufikisha  ujumbe wa matumaini  kwa watu wa Mexico, napenda kufikisha salaam zangu  za matashi mema  kwa ajili ya mazuri ya kiroho, kwako Mheshimiwa  Rais ,  kwa serikali na watu wote wa  Italia, na kwa moyo mkunjufu  nawapeni baraka zangu za kitume”

Aidha akipita anga la Ufaransa aliandika, ”nikiwa njiani kuelekea Mexico, ninakuhakikishia wewe Mheshimiwa Rais na raia wote wa Jamhuri ya Ufaransa, nitawakumbuka katika sala zangu , na kwa kila mmoja  apokeaa  Baraka za amani na furaha ”. Nchini Hispania alipeleka salaam kwa Mfalme na familia yake akisema,” ninapopita katiak anga la Hispania kuelekea Mexico , na kuhakikishia sala zangu kwako na watu wote wa Hispania  na kwa kila mmoja namwombea baraka za Mungu za amani na furaha.  Salaam kama hizo pia alizipeleka kwa Rais wa Jamhuri a Ureno na nchi zote anazopita juu yake.

Papa Francisko , katika ziara hii ya  Kitume ya siku sita nchini Mexico ,  12-18 Februari, 2016 akifuata nyayo za watangulizi wake Papa Yohane Paulo 11 na Papa Mstaafu Benedikto XVI, anakwenda  Mexico kukutana na wanakondoo wake wanaomsubiri kwa hamu , kubwa kuwapa ujumbe wa matumaini katika maisha yao ya kila siku.  

Anakwenda kutweka nyavu za ujumbe wa amani na maridhiano kati ya watu , si Jijini  Mexico tu lakini hata vitongojini , wanakoishi wazawa wengi asilia wa Mexico , na hasa  yenye  kuwa na sifa mbaya za uhalifu na mauaji,  kama ilivyo huko Ciudad Juarez eneo linalopakana na Mkoa wa Taxes Marekani . Anakwenda kuwa karibuni na watu na hasa maskini na wanaoonewa , kushirikishana nao mateso,  kufarijiana na ili kwa pamoja wajaribu  kupata jawabu linalofaa kurejesha  maisha ya haki na amani miongoni mwa watu wa Mexico.  Anakwenda kukutana na  viongozi  wa maeneo ambako  wananchi wananyanayaswa na kunyimwa haki zao kijamii, hasa kutokana na uwezo wa  mfumo mzito wa biashara haramu ya dawa  za kulevya  wenye kuhusishwa na  vurugu nyingi katika taifa la Mexico.  

 Papa akiwa njiani kuelekea  Mexico , atatua mjini Havana Cuba kwa  muda  ambako atakutana na Kiongozi Mkuu wa Upatriaki wa Kiorthodox wa Moscow na Urusi yote, Patriaki Kirill. Tukio linaloandika historia mpya ya viongozi wa Kanisa la Roma na Kanisa la Kiorthodox la Urusi  kukutana pamoja ana kwa ana .  








All the contents on this site are copyrighted ©.