2016-02-12 08:25:00

Msiwageuzie kisogo wagonjwa!


Mama Kanisa tarehe 11 Februari 2016 ameadhimisha Siku ya 24 ya Wagonjwa Duniani ambayo kwa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yameongozwa na kauli mbiu “Kujiaminisha kwa Yesu mwenye huruma kama Bikira Maria. Lolote atakalowaambia fanyeni”. Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la wahudumu katika sekta ya afya katika mahubiri yake katika tukio hili, huko Nazareti, amewataka waamini pamoja na wahudumu wa sekta ya afya kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai kwa kuwahudumia wagonjwa na wote wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali kama vile: vita, dhuluma na nyanyaso; ubaguzi na uhamiaji wa shuruti, wote hawa wanapaswa kuonjesha huruma , upendo na mshikamano wa dhati. 

Waamini kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria wanahamasishwa na Mama Kanisa kuguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya wagonjwa sehemu mbali mbali za dunia, ili waweze kusikiliza na kutekeleza kilio chao! Ibada ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya 24 ya Wagonjwa Duniani imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu. Waamini na watu wenye mapenzi mema waoneshe ujasiri wa kuwa karibu na wagonjwa, kwani wakati mwingine wagonjwa wanahitaji kusikia uwepo wa karibu wa ndugu na jamaa zao; watu ambao watakuwa tayari kumwonjesha mgonjwa upendo, huruma na mshikamano. Hi ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na wote hususan wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Familia ya Mungu ijenge na kukuza utamaduni wa huruma kwa wagonjwa, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa maisha. Wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na familia zina dhamana muhimu katika huduma ya huruma na uponyaji kwa wagonjwa. Huu ni wito na huduma ya huruma kwa wagonjwa, changamoto kwa waamini kutekeleza yote wanayoambiwa na Kristo, kama ilivyokuwa kwa wale wafanyakazi kwenye Arusi ya Kana ya Galilaya. Watu waguswe na mahangaiko ya wagonjwa, tayari kuwasaidia.

Mji wa Nazareti ni mahali ambapo waamini wanaweza kujifunza kwa makini Injili ya huruma ya Mungu. Ugonjwa ni Fumbo linaloandama maisha ya binadamu, kwa kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, Kristo anaweza kuwasaidia waamini kugundua maana ya mateso na mahangaiko yao, tayari kuyaunganisha na sadaka yake Msalabani. Bikira Maria kwa utayari wake alikubali kuwa ni Mama wa Huruma ya Mungu; akawa ni daraja kati ya wahitaji na Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo.

Bikira Maria anawaongoza waamini kujiaminisha kwa Kristo Yesu wakati wa raha na shida zao. Dhamana hii inapewa kipaumbele cha pekee wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hii ni fursa pia ya kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kwa pamoja waamini wa dini na madhehebu mbali mbali waweze kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika maisha na vipaumbele vya watu.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya 24 ya Wagonjwa Duniani aliwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua na kuona kwamba, kila hospital ina mahali pa kutunzia wagonjwa ni mahali muafaka pa kukuza na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kujenga amani; mahali ambapo mang’amuzi ya ugonjwa na huduma makini yanasaidia kubomoa kuta za utengano na ubaguzi wa aina mbali mbali!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.