2016-02-11 08:42:00

Jimbo kuu la Mombasa lapata "Majembe" ya huruma ya Mungu!


Askofu mkuu Martin Kivuva wa Jimbo kuu la Mombasa Kenya, katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya  huruma ya Mungu ametoa Daraja Takatifu la Upadre kwa Mashemasi watano na Daraja la Ushemasi wa mpito kwa Majandokasisi wawili; Wakleri hawa wametakiwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika huduma makini ya: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Huduma ya Upendo kwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Mombasa.

Ibada hii ya Daraja Takatifu la Upadre na Ushemasi, imefanyika hivi karibuni kwenye Kanisa la Bikira Maria, Bibi Yetu wa Matumaini, huko Taita, Taveta, Jimbo kuu la Mombasa. Familia ya Mungu Jimbo kuu la Mombasa, ilijumuika pamoja ili kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya wito wa Kipadre, unao endelea kuwahamasisha vijana wa kizazi kipya kufanya maamuzi machungu katika maisha yao kwa kujisadaka bila ya kujiachilia, ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya furaha na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Mapadre na Mashemasi hawa, tayari wameonesha ukarimu wa kujitoa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Askofu mkuu Kivuva amewataka wakleri hawa kuwa kweli mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wao. Amewashukuru wazazi na walezi, waliosaidia kuwafunda na kuwaunda watoto wao, kiasi kwamba, sasa wamekuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Daima wazazi na walezi wanapaswa kukumbuka kwamba, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu, haki na amani; ni mahali pa kuonja upendo, furaha, msamaha na matumaini.

Familia ziendelee kupandikiza mbegu ya miito mitakatifu, ili Kanisa liweze kupata wanandoa mahiri, makatekista safi na watakatifu pamoja na watawa na mapadre watakaojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wazazi na walezi wawe ni mfano bora wa kuigwa kwa watoto na majirani zao na kwa njia hii hata wao watakuwa ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo! Familia zinahamasishwa kuwa kweli ni shule ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama anavyohimiza Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Familia inayosali kwa pamoja, hiyo itashikamana na kudumu; itaweza kukabiliana na mawimbi mazito ya maisha.

Mapadre wapya ni: Gilbert Nyangala, Dennis Ogina, James Righa, Martin Mwandime na Stephen Safari. Wote hawa walisindikizwa na wazazi wao kwa madaha na mbwembwe; kwa vigelegele na vifijo, ili kudhihirisha nia yao ya kujitaka kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwatangazia watu wa Mungu Injili ya furaha, huruma na mapendo!

Na Sr. Bridgita Samba Mawasi,

Jimbo kuu la Mombasa, Kenya.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.