2016-02-10 14:15:00

Waonjesheni wagonjwa huruma na upendo wa Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kwa mahujaji na wageni, Jumatano ya majivu, tarehe 10 Februari 2016 amewakumbusha waamini kwamba, tarehe 11 Februari, Kanisa linafanya kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes na kwa namna ya pekee, Kanisa siku hii inaadhimishwa katika Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Siku ya 24 ya Wagonjwa Duniani inayongozwa na kauli mbiu “ Lolote atakalowambia fanyeni”!

Baba Mtakatifu anasema Mwaka huu, Kanisa linatafakari kwa namna ya pekee nafasi na dhamana ya Bikira Maria katika Arusi ya Kana ya Galilaya. Bikira Maria ni kioo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; ni ushuhuda wa wema wa Yesu Kristo mwenye huruma. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Bikira Maria, utawagusa na kuwaambata wale wote wanaowahudumia wagonjwa sehemu mbali mbali za dunia, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa wagonjwa. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwaalika wagonjwa waliokuwa wanamsikiliza wakati wa Katekesi yake kutoa mateso na mahangaiko yao kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani,  kwa wale wote ambao wako mbali na Mungu katika hija ya maisha yao ya kiroho!

Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya ndiye anayemwakilisha Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 24 ya Wagonjwa Duniani ambayo kwa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu inaadhimishwa mjini Nazareti. Maadhimisho haya yanajikita kwa namna ya pekee kabisa katika Liturujia kwa ajili ya kutoa Mpako Mtakatifu kwa wagonjwa na wazee, ili waweze kukabiliana na fumbo la mateso na mahangaiko yao ya ndani kwa imani na matumaini kwa Kristo Yesu.

Kuna kongamano la Kimataifa linaloendelea huko katika Nchi Takatifu, kwa kuangalia matatizo, fursa na changamoto wanazokabiliana nazo wagonjwa na wadau mbali mbali katika kuwahudumia wagonjwa ambao wako kufani. Hapa kwa namna ya pekee suala zima ni kuangalia utakatifu wa maisha ya binadamu, kanuni maadili na utu wema. Kongamano hili linawashirikisha mabingwa katika huduma ya wagonjwa walioko kufani. Kwa namna ya pekee, waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika Nchi Takatifu wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya ambayo pia yanafanyika kwenye Makanisa mahalia! Hii ni siku muhimu sana ya kuwaonesha wagonjwa hasa waliokufani uso wa huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.