2016-02-10 07:11:00

Wamissionari wa huruma ya Mungu: Mambo ya kuzingatia!


Wamissionari wa huruma ya Mungu wanaalikwa kutambua kwamba, wanatekeleza kwa dhati kabisa umama wa Kanisa anayezaa watoto katika imani; anayewalisha kwa Neno na Sakramenti; Mama mwenye huruma anayewahamasisha watoto wake kutubu na kumwongokea Mungu. Wamissionari wa huruma ya Mungu wanapaswa kutambua ile kiu ya mdhambi inayomsukuma kuomba huruma na msamaha, matunda ya neema ya Mungu inayofanya kazi ndani mwake, Aibu ya dhambi inaweza kumpelekea mwamini kukimbilia huruma ya Mungu!

Haya ni kati ya mambo makuu matatu yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Wamissionari wa huruma ya Mungu 1, 071, alipokutana nao kwa mara ya kwanza mjini Vatican Jumanne tarehe 9 Februari 2015. Baba Mtakatifu anawakumbusha Wamissionari hawa kwamba, wanatumwa  kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Wanapaswa kuonesha ukaribu wa upendo na uwepo endelevu wa Mungu kwa waja wake. Wao ni msaada mkubwa kwa waamini wanaotaka kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Wamissionari hawa wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa Umama wa Kanisa, Kanisa ambalo linajipatia watoto wapya  katika imani na kuwalisha katika imani kwa njia ya Neno na Sakramenti; ni Mama anayetaka watoto wake watubu na kumwongokea Mungu, ili kupyaisha maisha yao. Mdhambi atambue kwamba Mama Kanisa anamkaribisha na kumpenda. Mambo haya msingi yasipozingatiwa yanaweza kusababisha madhara makubwa kwa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Mwamini atashindwa kujisikia kuwa ni sehemu ya Jumuiya ya waamini.

Waamini wakumbuke kwamba, daima wanapoingia kwenye kiti cha huruma ya Mungu, wanapokelewa na Kristo Yesu anayewasikiliza na kuwasamehe dhambi zao na hatimaye, kuwapatia amani; Mapadre ni vyombo vya huruma ya Mungu, vinavyopaswa kusamehewa kabla ya kusamehe. Mdhambi anapoungama, Padre atambue kwamba, kabla ya yote ni mdhambi, kumbe anapaswa kuwa ni chombo cha huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu amewakumbusha tarehe 21 Septemba 1953 alipoungama kwa mara ya kwanza, alipoonja upendo na huruma ya Mungu katika maisha yake.

Baba Mtakatifu anasema jambo la pili ambalo Wamissionari wa huruma ya Mungu wanapaswa kukumbuka ni ile kiu ya msamaha inayooneshwa na mdhambi anayekimbilia kwenye kiti cha huruma ya Mungu, matunda ya neema ya Mungu inayofanya kazi ndani mwake, kiasi cha kujisikia kwamba, kweli anahitaji uwepo wa Mungu na hii ndiyo chemchemi ya wongofu na mageuzi ya ndani inayomsukumza mwamini kujiwekea lengo la kutotenda dhambi tena. Wamissionari wa huruma ya Mungu wawe makini kuguswa hata na yale ambayo hayakusemwa na muungamaji. Wakati mwingine muungamaji anashindwa kujieleza barabara, Wamissionari wa huruma ya Mungu walitambue hili, kwani wao ni vyombo tu, lakini aneyesikiliza na kusamehe ni Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, jambo la tatu ambalo angependa kukazia ni aibu anayokumbana nayo mdhambi pale anapokimbilia kiti cha huruma ya Mungu. Ni aibu ya dhambi alizotenda na zaidi kwamba, anapaswa kuziungama kwa mtu mwingine tena. Aibu ni jambo linalomtendea mtu katika ubinadamu wake, changamoto ya kuheshimu na kusaidia kutia moyo mwamini anayekimbilia huruma ya Mungu. Aibu wakati mwingine inampelekea mtu kushindwa kusema, kama Maandiko Matakatifu yanayovyosimulia, pale Adamu na Hawa walipojikuta wako tupu na jambo la kwanza walilotenda ni kujificha ili wasionekane na Mungu. Watoto wa Nuhu waliona utupu wa Baba yao, wakaamua kumfunika, ili kumrudishia tena utu na heshima yake.

Baba Mtakatifu anawakumbusha Wamissionari wa huruma ya Mungu kwamba, wanapokuwa katika kiti cha huruma ya Mungu, mbele yao kuna mwamini ambaye yuko tupu! Anayeona aibu ya dhambi alizotenda, ni mtu anayetamani kupokelewa, kusikilizwa na kuondolewa dhambi na kupewa msamaha na huruma ya Mungu. Wamissionari wa huruma ya Mungu kamwe wasiwe ni Mahakimu watakatili kiasi cha kushindwa kutambua kwamba, hata wao pia ni wadhambi, kumbe wanapaswa kuwarudishia wadhambi utu na heshima yao kama watoto wa Mungu kwa njia ya huruma ya Mungu mintarafu Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, utakatifu wa maisha ni chachu muhimu sana katika kuleta mageuzi ndani ya Kanisa. Utakatifu unarutubishwa kwa upendo kwa kuwasindikiza wanyonge na wadhaifu kwa njia ya huruma inayofariji na kupenda. Wamissionari wa huruma ya Mungu waoneshe upendo wa Baba mwenye huruma. Watakatifu Padre Pio wa Pietrelcina na Padre Leopoldo pamoja na Wakleri ambao wameonesha ushuhuda wa huruma ya Mungu kwa watu wao, wawe ni mfano bora wa kuigwa, tayari kuwaonjesha watu wa Mungu huruma ya Baba wa milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.