2016-02-10 09:09:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 24 ya Wagonjwa Duniani 2016


Katika Nchi Takatifu kila hospitali na nyumba ya kutunza wagonjwa panaweza kuwa ni mahali muafaka pa watu kujenga utamaduni wa kukutana na kudumisha amani; mahali ambapo magonjwa na mahangaiko ya mwanadamu yanapata kitulizo kwa huduma makini inayotolewa na wahudumu katika sekta ya afya pamoja na wagonjwa kuhudumiwa kwa upendo na udugu na wale wote wanaowazunguka. Hii ni changamoto na mwaliko wa kuondokana na kishawishi cha mipasuko na utengano unaoweza kujitokeza katika maisha ya watu!

Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko anavyosema katika ujumbe wake kwa siku ya 24 ya Wagonjwa Duniani ambayo kwa Mwaka 2016 inaadhimishwa mjini Nazareti, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Fanyeni yale atakayowaambia”. Hii ni changamoto ya kujiaminisha kwa Yesu Kristo, chemchem ya huruma ya Baba kama alivyofanya Bikira Maria wakati wa arusi ya Kana ya Galilaya, Yesu alipotenda muujiza wake wa kwanza kwa ombi lililotolewa na Bikira Maria. Kilele cha maadhimisho haya ni tarehe 11 Februari 2016 wakati Mama Kanisa anapoadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes.

Nazareti ni mji ambamo Neno wa Mungu alifanyika mwili na hapo akaanza kazi ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwani Roho wa Bwana alikuwa juu yake na akampaka mafuta ili kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao na vipofu kupata kuona tena, wanaoonewa kuachiliwa huru na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa (Lk. 4:18- 19).

Ugonjwa ni changamoto ambayo ina beba maswali mengi katika maisha ya mwanadamu ili kutafuta maana na thamani ya maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anasema, imani inaweza kutikiswa au kumsaidia mgonjwa kupata maana ya ndani kabisa ya mateso na mahangaiko yake ya kibinadamu, kiasi cha kumvuta kuwa karibu na Yesu anaendelea kuandamana na wafuasi wake, akiwa ameelemewa na Msalaba. Bikira Maria alikuwa na jicho la kimama, akaona mateso na mahangaiko ya wanaarusi wa Kana ya Galilaya, akachukua uamuzi wa kumwendea Yesu na kumwambia “hawana divai”. Yesu alimwambia Mama yake kwamba, saa yake ilikuwa bado haijawadia, lakini kwa ombi la Bikira Maria akawajalia maarusi kupata divai njema zaidi katika arusi yao, mambo yakafana zaidi!

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, arusi ya Kana ya Galilaya ni sura ya Kanisa na kiini cha Kanisa ni Kristo Yesu mwenyewe anayetenda miujiza kama kielelezo cha huruma kwa binadamu huku akiwa amezungukwa na Mitume wake; matunda ya kwanza ya Jumuiya mpya; ambamo pia alikuwepo Bikira Maria anayesali pamoja na Kanisa. Ni Mama anayeshiriki furaha ya watu wa Mungu, anayewaombea kwa Mwanaye wa pekee Yesu Kristo.

Kwa hakika Bikira Maria ni jicho la upendo na huruma ya Mungu kwa watu mbali mbali kama Yesu mwenyewe alivyofanya kwa kuwalisha wenye njaa, kuwaponya wagonjwa na kuwaondolea watu dhambi zao. Bikira Maria anawasaidia wamini kufungua malango ya mioyo yao, tayari kupokea huruma ya Mungu katika maisha yao, ili wao pia wawe na ujasiri wa kuwashirikisha wengine huruma hii! Bikira Maria ni kielelezo cha faraja kwa watu wenye shida na mahangaiko mbali mbali ya maisha. Yesu katika maisha na utume wake aliwarudishia watu heshima na utu wao pamoja na kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu, yote haya yanaonesha nguvu ya Kimasiha na huruma ya Baba wa milele.

Kwa njia ya Bikira Maria, waamini wanajifunza upendo na huruma ya Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku, kwani anapenda kuwaangalia kwa jicho lenye huruma na mapendo ili kuweza kuwashirikisha wote hawa katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Imani inayoboreshwa kwa mapendo anasema Baba Mtakatifu, inawawezesha waamini kuomba amani na utulivu wa ndani unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, zawadi ambayo kamwe Mwenyezi Mungu hawezi kuwanyima waja wake.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba, kwenye arusi ya Kana ya Galilaya walikuwepo watumishi, ambao walishirikiana na Yesu katika kufanikisha muujiza ule wa kwanza uliorejesha kicheko cha furaha na matumaini kwa wanarusi wa Kana ya Galilaya. Binadamu wanashirikishwa pia katika huduma inayoendeleza mchakato wa kazi ya ukombozi, mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo vya huduma, huku wakiendelea kumuiga Kristo aliyekuja si kutumikiwa bali kutumikia na kutoa maisha yake ili yawe ni fidia ya wengi.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa pasi na manung’uniko, kwa kutambua kwamba, wakati mwingine huduma hii ina changamoto zake, lakini waamini waendelee kuwa ni vyombo vya huduma kwa wagonjwa na wenye shida zaidi kwa kuchangia furaha na ustawi wa wagonjwa kwa hali na mali kama njia ya kubeba vyema Misalaba na kumfuasa Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa makini ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani; ili kufahamiana, kuheshimiana na kusaidiana ili kuondokana na ubaguzi na utengano usiokuwa na mvuto wala mashiko. Hospitali na nyumba za kuwahudumia wagonjwa ziwe ni mahali pa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana.

Watakatifu Marie Alphonsine Danil Ghattas na Maria wa Yesu Mteswa Baouardy kutoka Nchi Takatifu; mashuhuda wa unyenyekevu, umoja, huduma na majadiliano ya kidini wasaidie kukoleza na kumwilisha tunu hizi msingi katika uhalisia wa maisha ya watu huko kwenye Nchi Takatifu. Baba Mtakatifu anawaalika wafanyakazi wote katika sekta ya afya kuiga mfano wa Bikira Maria, Mama wa huruma katika utekelezaji wa majukumu yao, ili kuwawezesha wagonjwa kuonja tena furaha, amani na utulivu wa ndani hata katika magonjwa na mahangaiko yao! Wafanyakazi hawa wawaoneshe wagonjwa Sura ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.