2016-02-10 15:23:00

Bonde la Bura, Jimbo kuu la Mombasa ni mahali patakatifu!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa ya pekee kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi kuitafuta, kuiambata na kuwashirikisha wengine, kwa njia ya toba, wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho wa kweli unaobubujika kutoka katika moyo unaoguswa na huruma ya Mungu! Hayo yamedhihirishwa hivi karibuni, wakati Askofu mkuu Martin Kivuva wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya alipozindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu Jimbo kuu la Mombasa, katika Ibada iliyoadhimishwa kwenye Kanisa Bikira Maria wa Matumaini, Parokia ya Bura, huko Taita nchini Kenya!

Tukio hili la pekee katika maisha na utume wa Kanisa, Jimbo kuu la Mombasa, Askofu mkuu Kivuva alitoa Daraja la Ushemasi kwa Majandokasisi wawili, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa njia ya Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma kadiri ya Daraja lao. Askofu mkuu Kivuva pia alitumia fursa hii kufungua Lango la Huruma ya Mungu, tayari kwa mahujaji kutoka Jimbo kuu la Mombasa kukimbilia huruma ya Mungu.

Itakumbukwa kwamba, kwa mara ya kwanza Jimbo kuu la Mombasa lilizundua maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu hapo tarehe 29 Januari 2016, Askofu Mkuu Kivuva alipovishwa rasmi Palio Takatifu, alama ya umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro, tukio ambalo liliongozwa na Askofu mkuu Charles Bavo, Balozi wa Vatican nchini Kenya. Ili kuwawezesha waamini kuadhimisha kikamilifu Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Askofu mkuu Kivuva ameamua kufungua Malango ya Huruma ya Mungu katika maeneo kadhaa, ili kutoa nafasi kwa waamini kukimbilia huruma ya Mungu kadiri ya nafasi na uwezo wao.

Askofu mkuu Kivuva anasema, eneo la Bura ni muhimu sana katika historia na maisha ya Kanisa Katoliki nchini Kenya, kwani hapa kilikuwa ni kituo cha kwanza kwa Wamissionari kutua nanga ya imani, matumaini na mapendo nchini Kenya, baada ya kuwasili Mombasa. Kanisa hili lina umri wa miaka 124 tangu lilipojengwa na kutoka katika eneo hili, Ukristo ukaenea sehemu mbali mbali za Kenya, leo hii Wakristo wanaalikwa kwa namna ya pekee kuwa ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha. Hapa pia ni nyumba Mama ya Shirika la Watawa wa Mtakatifu Yosefu Jimbo kuu la Mombasa, lililoanzishwa kunako mwaka 1941.

Bonde la Bura ni mahali patakatifu, chemchemi ya Ukristo na changamoto ya kuendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo. Eneo hili liwe ni mahali pa sala na tafakari, mahali pa waamini kupyaisha upya maisha yao na kwamba, kila mwaka ifikapo tarehe 24 Septemba, Familia ya Mungu Jimbo kuu la Mombasa itakusanyika kumshukuru na kumwomba Mungu katika safari ya maisha yake ya kiroho! Huu ni mwanzo wa changamoto za kumwilisha huruma ya Mungu katika matendo!

Na Sr. Bridgita Samba Mwawasi.

Jimbo kuu la Mombasa, Kenya.








All the contents on this site are copyrighted ©.