2016-02-09 08:11:00

Papa atoa heshima zake kwa Masalia ya Watakatifu Padre Pio na Leopoldo


Baba Mtakatifu Francisko ni kati ya mahujaji na waamini waliotembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kusali mbele ya Masalia ya Watakatifu Padre Pio wa Pietrelcina na Padre Leopoldo Mandic. Baba Mtakatifu katika siku za hivi karibuni amekutana na kusali pamoja na wanachama wa utume wa Sala wa Mtakatifu Padre Pio. Jumanne, tarehe 9 Februari 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya watawa wa Mashirika ya Kifranciskani kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko alipitia Lango la Sala huku akiwa amesindikizwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilsihaji Mpya pamoja na Askofu mkuu Michele Castoro wa Jimbo kuu la Manfredonia-Vieste - San Giovanni Rotondo. Baba Mtakatifu alipofika mbele ya Altare, alipewa sala kwa ajili ya watakatifu hawa na kwa kitambo akasali na kutafakari matendo makuu ya Mungu aliyowakirimia watu wake kwa njia ya watakatifu hawa wawili, waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwashirikisha watu huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho.

Baba Mtakatifu kama mahujaji wengine alikaa kimya na kushirikiana na waamini wengine waliokuwa wanasali Rozari Takatifu, muhtasari wa Injili ya Kristo, kielelezo cha Huruma ya Mungu kwa waja wake. Rozari hii imeongozwa na wanafunzi kutoka Kanda ya Wakapuchini wa “Sant’Angelo” kutoka Mkoa wa Puglia. Baadaye, Baba Mtakatifu pia alishiriki katika sala iliyotungwa kwa ajili ya tukio hili na Kardinali Angelo Comastri, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Wakati Baba Mtakatifu akitoka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alisimama kwa kitambo ili kumsalimia Mtoto aliyekuwa amelazwa kwenye kitanda cha wagonjwa akiwa na mama yake! Akasalimiana pia na watawa wawili wazee kutoka Jumuiya ya Wakapuchini wa San Giovanni Rotondo. Waamini na mahujaji wanaendelea kutoa heshima zao kwa Masalia ya watakatifu Padre Pio na Padre Leopoldo Mancic; Jumatano ya Majivu hadi Alhamisi tarehe 11 Februari 2016 Masalia ya watakatifu hawa yatakaporejeshwa katika maeneo yake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.