2016-02-08 09:47:00

Papa : Imani kwa Neno la Yesu huzaa matunda tele


Jumapili, Baba Mtakatifu Francisko akihutubia maelfu ya mahujaji na wageni waliofika katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro , kwa nia ya kusali pamoja nae sala ya Malaika wa Bwana, kabla ya sala hiyo,  alitoa tafakari fupi  juu ya somo la Injili,  ambalo  linazungumzia wito wa  Yesu kwa  wafuasi wake wa kwanza, akiwa kando ya  Ziwa Galilaya. Wafuasi hao wa kwanza ambao walikuwa wavuvi , wakiwa  katika hali ya kukata tamaa baada ya kuvua usiku mzima bila kupata samaki,  walianza kuweka nyavu zao sawa, ili warejee makwao .  Yesu anaingia katika mashua  ya Simon Petro na  kuhubiri  umati wa watu waliokusanyika katika pwani ya Ziwa Galilaya .

Baada ya kuhutubia  Yesu anamwambia  Petro, kutweka nyavu kilindini, ili wapate samaki. Na Petro anamjibu Yesu , kwamba wamefanya hivyo usiku wote na hawakupata kitu , lakini akaonyesha imani yake kwa Yesu na kusema , kwa maneno yako, tunaweka tena nyavu kilindini.Papa anasema  imani ya Petro kwa maneno ya Yesu iliwapa zawadi ya samaki wengi , waliotaka hata kukata nyavu!

Wakiwa katika hali ya kushangalia  maajabu hayo, Petro alijiona mnyonge na kuanguka  miguuni pa Yesu akisema, "Ondoka mbele yangu Bwana, kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi.  Petro,  alieleza Papa, anapata kufahamu kwamba Yesu ni Bwana na anapata hisia kali  kwamba , hawasikustahili  kuwa mbele za Bwana. Lakini Yesu anamwambia: "Usiogope, tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu". Papa alisema  Yesu hakuondokana kumwacha Petro katika dhambi zake , bali alimtakasa na kumfanya  kuwa mfuasi wake, upendo wa Yesu unakuwa zaidi ya daktari anayemhudumia mgonjwa na kumwacha.

Papa alisema , maneno ya Yesu kwa Petro na wanafunzi wengine , ni kiini cha huduma ya Yesu  na utume wa Kanisa.  Na alifafaanua kwamba, kwenda  kuvua watu, wake kwa waume haina maana ya  kuwalazimisha wengine kumwongokea Yesu,  lakini ni  kurejesha heshima na uhuru wao kupitia msamaha wa dhambi. Hicho ndicho  kiini cha Ukristo.  Ni  kushiriki upendo  unaotolewa bure na kuendelea kukua ndani na  Mungu kwa njia ya ukarimu na huruma kwa watu wote.

Baada ya hotuba hiyo , Papa alisali sala ya  Malaika wa Bwana. Na alikamilisha tukio hili kuizungumzia kidogo pia  ziara yake ya kitume nchini  Mexico na Cuba , anayotazamia kuianza mwishoni mwa wiki hii, ambamo pia anatazama  kukutana na  Patriaki Kirill, Mkuu wa Kanisa  Kiotodosi  la Moscow na Urusi yote.  Papa pia aliwakumbusha waamini katika  Jumatatu  katiak sala zao kuwakumbuka wahanga wote wa utumwa mambo leo.  Mama Kanisa , ameadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Bakhita, kwa kuwaombea wote wanaoishi katika hali za udhalimu wa utumwa mambo leo kinyume.  Pia aliomba   wakati huu wa mapambazuko  ya mwaka mpya , amani na utulivu vitawale kwa wote na  kwa namna ya kipekee alilitaja  Taifa la China ambalo Jumatatu hii, limeadhimishwa Siku Kuu ya Mwaka Mpya , kwa mujibu Kalenda ya China.  

Aidha  Papa , kwa mara ingine alitoa ombi kwa  Jumuiya ya kimataifa, ione haja ya kutenda kidharura, kurejesha  amani nchini Syria. Aliomba kila juhudi ifinyike kufanikisha mazungumzo ya pamoja kwa pande zote zinazo husika katika mzozo huu wa Syria, waketi pamoja katika meza ya mazungumzo na kutoa jibu moja muafaka  kwa wote,  linaloweza sitisha ukatili unaofanyika hasa kwa raia wanyonge  wasiokuwa na usemi nchini Syria .  Kwa ajili hiyo, Papa aliomba  sala  za  wote , ziwakumbuke raia hawa wa Syria waliojikuta wamezingira na mapiganoya kivita, yanayo kuacha kila kitu  kwa hofu wakikimbia dhuluma za vita na  kupoteza maisha yao.

Papa aliomba “mshikamano na ukarimu”,  hasa katika upatikanaji wa mahitaji ya lazima kwa  wakimbizi hawa,  na kuhakikisha wanaishi katika hali ya maisha yenye  heshima.. Na wakati  huohuo  jumuiya ya kimataifa ifanye kazi kwa haraka zaidi, kupata  ufumbuzi  wa vita hivyo , kupitia njia ya mazungumzo . Alisisitiza ni tu majadiliano katika meza moja yanayoweza  kupata ufumbuzi katika kinzani za kisiasa na kuhakikisha  uwepo wa maridhiano na amani kwa taifa hilo la Syria.

Papa Francisko alikamilisha ombi lake kwa Jumuiya ya kimtaifa akiomba pia watu wote kusali kwa ajili ya amani  nchini Syria,na kuwa tayari kuwapokea wakimbizi wanaotafuta hifadhi na aliomba maombezi ya Bikira Bikira Maria, Malkia wa amani. 








All the contents on this site are copyrighted ©.