2016-02-06 16:36:00

Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni nguzo ya majadiliano ya kiekumene!


Wajumbe wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo hivi karibuni wamehitimisha mkutano wao wa mwaka pamoja na wajumbe wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni huko Geneva, Uswiss. Mkutano huu umefanyika wakati Jumuiya ya Kimataifa ikiwa inaadhimisha juma la maridhiano ya kidini lililotangwa na Umoja wa Mataifa. Mkutano huu umekuwa ni fursa ya kusali, kutafakari na kubadilisha taarifa mintarafu shughuli mbali mbali zilizofanyika katika kipindi cha mwaka 2015, tayari kupanga mikakati itakayotekelezwa na pande hizi mbili kwa mwaka 2016.

Wajumbe wa mabaraza haya mawili kwa miaka ya hivi karibuni wameshirikiana kwa karibu sana, hususan kwa kuandika waraka wa pamoja kuhusiana na ushuhuda wa Wakristo katika ulimwengu wenye dini nyingi. Ushauri wa kimaadili uliochapishwa kunako mwaka 2011 ili kutoa ushauri na kushiriki katika matukio au miradi mbali mbali inayoandaliwa na mabaraza haya. Itakumbukwa kwamba, Mwaka 2015 uligubikwa kwa kiasi kikubwa na maadhimisho ya Tamko la Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusiana na majadiliano ya kidini “Nostra aetate”.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linatambua Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kama tukio muhimu sana katika kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini. Mkutano mwa waka 2016 imekuwa ni fursa ya kupembua kwa kina na mapana ushirikiano wa dhati kati ya Mabaraza haya mawili mintarafu mwanga na matamanio ya kutaka kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene kadiri Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walivyokazia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.