2016-02-05 16:21:00

Vatican inazihamasisha nchi wahisani kuchangia huduma kwa wakimbizi!


Kanisa Katoliki litaendelea kuonesha mshikamano wa upendo na wananchi wa Syria kwa kutoa msaada wa hali na mali kwa wale wanaoteseka. Hayo yamesemwa na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, Alhamisi tarehe 4 Februari 2016 huko mjini London wakati wa mkutano wa nchi wafadhili wa Syria. Huu ni mkutano uliokuwa unalenga pamoja na mambo mengine kuendelea kuunga mkono juhudi za Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambao kwa sasa wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Nchi wahisani zinaombwa kuchangia fedha kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi wanaohifadhiwa kwenye nchi jirani. Kanisa kwa upande wake linatoa msaada kwa wananchi wote bila ubaguzi, daima kipaumbele cha kwanza kikiwa ni kwa wahitaji zaidi. Katika kipindi cha miaka mitano ya vita nchini Syria kumekuwepo na madhara makubwa kwa maisha ya watu na imani zao, hususan wakristo wanaodhulumiwa na kunyanyaswa. Kutokana na hali kama hii, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kuiangalisha Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kuwatetea na kuwalinda Wakristo huko Mashariki ya Kati.

Askofu mkuu Gallagher anaendelea kufafanua kwamba, Vatican kwa kupitia Mashirika yake ya misaada kimataifa, kikanda na kitaifa imeongeza kiwango cha fedha kwa ajili ya msaada kwa wananchi wa Syria. Vatican inapenda kuzialika nchi wahisani kushikamana kwa dhati ili kuchangia msaada kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji; kwa Jumuya na nchi zile ambazo zinatoa hifadhi kwa watu hawa kwani kwa kiasi kikubwa zinaathirika sana. Nchi hizi ni kama vile: Yordan, Lebanon, Iraq, Uturuki na Misri.

Kanisa Katoliki katika kipindi cha mwaka 2015 kwa kusaidiana na waamini na wafadhili mbali mbali kutoka duniani kote, limechangia kiasi cha dolla za Kimarekani millioni 150, fedha ambazo zimewasaidia watu zaidi ya millioni 4. Kanisa Katoliki limeelekeza nguvu zake zaidi katika masuala ya elimu, chakula, afya na makazi. Kiasi kingine cha dolla za Kimarekani millioni 12 zimetumika kwa ajili ya kutoa huduma ya maji safi na salama pamoja na usafi, bila kusahau msaada wa kisaikolojia na kijamii, mambo muhimu kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.