2016-02-05 15:59:00

Usipende kujitwalia sifa na utukufu wa watu wengine!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Ijumaa tarehe 5 Februari amesema, Yohane Mbatizaji ni kati ya watu mashuhuri sana aliyezaliwa na mwanamke na ni kati ya watakatifu wa Mungu aliyesimamia ukweli, akaushuhudia hata kukatwa kichwa. Wanafunzi wa Yohane waliposikia yaliyokuwa yametendeka wakaenda kuuchukua mwili wa Yohane Mbatizaji ili kumzika. Hivi ndivyo maisha ya Nabii na Daraja kati ya Agano la Kale na Agano Jipya yalivyomiminwa, lakini akabahatika kuona matumaini ya Waisraeli kwa kuzaliwa Kristo Mkombozi wa dunia.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake ameendelea kupembua kwa kina na mapana maisha ya Yohane Mbatizaji, kwa kuangalia moyo wake, huyu ambaye alipaaza sauti Jangwani, akawabatiza watu Ubatizo wa toba na maondoleo ya dhambi; akawa ni shuhuda wa Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za dunia. Hata akiwa gerezani bado wengi hawakuiamini minyororo iliyokuwa imemfunga Yohane Mbatizaji.

Yohane Mbatizaji alikuwa na maswali mengi kichwani mwake, mambo ambayo yalimtesa zaidi kuliko hata minyororo waliyokuwa wamemfunga. Alimwona Kristo Masiha lakini si kama alivyowaza na kufikiri, kiasi hata cha kuwatuma wafuasi wake kwenda kumhoji Yesu ikiwa kama ndiye aliyekuwa anasubiriwa na Waisraeli! Kwa maswali haya akaonja upweke  na mateso ya ndani, akapungua kiroho na kimwili. Yohane Mbatizaji alijisadaka kwa Mungu bila kutafuta utukufu wake binafsi na kwa njia hii akamwandalia Kristo Yesu njia ya kufuata; akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujisomea na kutafakari kwa kina Injili ya Marko, Sura ya sita ili kuona jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anashinda kwa kishindo si katika mtindo wa kibinadamu! Waamini wawe na ujasiri wa kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya unyenyekevu kama aliokuwa nao Yohane Mbatizaji bila kujitwalia sifa na utukufu wa watu wengine. Wakristo waoneshe katika maisha yao, nafasi ya Kristo anayekua na kuongezeka siku kwa siku na wao wenyewe wakishuka taratibu hadi kupotea kabisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.