2016-02-05 16:59:00

Papa Francisko atembelea Mabaraza ya Kipapa!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 4 Februari 2016 ametembelea Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya ambalo limepewa dhamana ya kuratibu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, ambalo limeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, muhimu sana katika kukoleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika: ukweli, huduma, sala na damu ya mashuhuda wa imani ya Kikristo.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwatembelea na kuwatia moyo kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya katika kuratibu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu ametoa changamoto na chachu ya Uinjilishaji mpya unaojikita katika toba na wongofu wa ndani; katekesi makini na endelevu inayofumbata: Imani, Sakramenti, Amri za Mungu na Maisha ya Sala.

Hizi ni kati ya changamoto kubwa kwa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Hizi pia ni mada zinazoshughulikiwa moja kwa moja na Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya. Baba Mtakatifu amewasikiliza na kujibu maswali ya baadhi ya wafanyakazi wa Baraza hili. Baba Mtakatifu Francisko ametembelea Mabaraza haya ya Kipapa wakati huu Roma ukiwa umesheheni umati mkubwa wa waamini wanaofika kusali na kutoa heshima zao kwa Mtakatifu Padre Pio na Mtakatifu Leopoldo Mandic; wamissionari wa huruma ya Mungu, waliotumia muda wao mwingi kwa ajili ya kuwaondolea watu dhambi zao, changamoto na mwaliko kwa waamini kukimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya toba na maungamo ya dhambi zao, ili wao pia wawe tayari kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa jirani zao.

Baba Mtakatifu anasema, watakatifu hawa wawili ni mashuhuri sana ndani ya Kanisa kutokana na mchango wao katika ustawi na maendeleo ya watu kiroho. Baba Mtakatifu anasema ana ibada kwa Mtakatifu Leopoldo Mandic ndiyo maana Jumatano ya Majivu, anataka kuwakabidhi na kuwaaminisha wamissionari wa huruma ya Mungu, tayari kuwaonjesha watu huruma na upendo wa Mungu. Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa kwa waamini kukimbilia kwenye kiti cha huruma ya Mungu na Mapadre, waiadhimishe Sakramenti hii kwa ibada, nidhamu na moyo mkuu, kwa kuonesha ukarimu, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.