2016-02-05 16:37:00

Dolla billioni 7 zinahitajika kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon amewashukuru na kuwapongeza wafadhili mbali mbali wanaoendelea kujioa mhanga kwa ajili ya kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria na Ukanda wa Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Bwana Ban Ki-Moon ameyasema haya, Alhamisi, tarehe 4 Februari 2016 alipokuwa anawahutubia wawakilishi wa nchi wafadhili wa Syria na Ukanda wa Mashariki ya Kati huko London.

Inakaribia kugota miaka sita tangu mtutu wa bunduki ulipoanza kulindima nchini Syria na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa ina wajibu mkubwa katika kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Mashariki ya Kati. Umoja wa Mataifa uanapania kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kisiasa, ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu huko Syria, ili kutoa nafuu kwa mamillioni ya watu wanaoteseka kutokana na vita, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anakaza kusema kiasi cha Dolla billioni 7 kinahitajika kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji kwa mwaka 2016. Kiasi hiki cha fedha kimeongezeka maradufu. Bado kuna haja ya kuwa na mfuko maalum wa kuwasaidia wananchi wa Syria kwa siku za usoni hususan katika masuala ya elimu na afya. Jumuiya ya Kimataifa inayo dhamana pevu ya kuhakikisha ulinzi na usalama kwa wakimbizi pamoja na kuwapatia chakula na malazi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anafafanua kwamba, hali ya Syria kwa sasa ni tete sana; hakuna suluhu ya kijeshi, bali wadau mbali mbali wanapaswa kuonesha utashi wa kisiasa kwa kujikita katika majadiliano ya kisiasa, ili kuokoa watu kutokana na maafa haya yanayoendelea kuwasibu. Umoja wa Mataifa unawashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wa Mashirika ya misaada kimataifa huko Syria, watu wanaohatarisha maisha yao kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi huko Mashariki ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.